1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Blinken aondoka Mashariki ya Kati bila mafanikio

8 Februari 2024

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, ameondoka Mashariki ya Kati Alhamisi wakati tofauti za wazi kati ya nchi yake na Israel zikiwa katika kiwango kibaya zaidi tangu kuanza kwa vita vya Israel na Hamas

https://p.dw.com/p/4cBfi
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken (Kushoto) na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wasalimiana mjini Jerusalem mnamo Februari 7, 2024
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken (Kushoto) na waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: GPO/Anadolu/picture alliance

Akihitimisha ziara yake ya mataifa manne Mashariki ya Kati, hii ikiwa ziara ya tano katika eneo hilo tangu kuzuka kwa vita hivyo, Blinken anarudi Marekani bila mafanikio yoyote baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kusema kwamba vita hivyo vitaendelea hadi pale Israel itakapopata ushindi.

Soma pia:Netanyahu ayakataa mapendekezo ya Hamas

Netanyahu pia amelipinga moja kwa moja pendekezo la Hamas la usitishwaji mapigano.

Uhusiano kati ya Marekani na Israel watiliwa mashaka

Uhusiano kati ya Israel na mshirika wake mkuu, Marekani, umekuwa wa kutiliwa mashaka kwa miezi kadhaa, lakini hatua ya Netanyahuya kupuuzilia mbali hadharani mpango ambao Marekani imeutaja kuwa na tija, angalau kama sehemu ya mwanzo ya mazungumzo zaidi, imeonesha mgawanyiko huo.

Marekani bado ina matumaini ya kupata suluhisho kwa mzozo wa Gaza

Blinken na maafisa wengine wa Marekani wamesema bado wana matumaini kwamba huenda kukawa na ufanisi katika malengo yao makuu ya kuboresha hali ya kibinaadamu kwa raia wa Palestina, kuwezesha kuachiwa huru kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas, kujiandaa kwa Gaza baada ya vita na kuzuia vita hivyo kuenea.

Biden kuzungumzia mzozo wa Gaza na mfalme wa Jordan 

Ikulu ya White House ya Marekani imesema kuwa Rais Joe Biden atafanya mazungumzo na mfalme wa Jordan mjini Washington mnamo Februari 12.

Wanajeshi wa Israel wafanya operesheni katika Ukanda wa Gaza mnamo Jnauari 21, 2024 wakati mapigano yanayendelea kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas
Wanajeshi wa Israel wafanya operesheni katika Ukanda wa GazaPicha: ISRAEL DEFENSE FORCES/REUTERS

Katika taarifa yake, msemaji wa White House, Karine Jean-Pierre, amesema leo kuwa viongozi hao wawili watazungumzia hali inayoshuhudiwa katika Ukanda wa Gaza na juhudi za kupata suluhisho la kudumu kumaliza mapigano yanayoendelea katika eneo hilo.

Jeshi la Israel lafanya mashambulizi katika mji wa Rafah

Jeshi la Israel limefanya mashambulizi Alhamisi katika mji wa Rafah katika mpaka wake wa Kusini ambao zaidi ya nusu ya idadi ya wakaazi wa Gaza wamekimbia kupata hifadhi.

Soma pia:Blinken azungumza na Israel juu ya pendekezo la Hamas

Mashirika ya misaada yameonya kuhusu janga la kibinaadamu iwapo Israel itatimiza kitisho chake cha kuingilia moja kati ya maeneo ya mwisho katika Ukanda wa Gaza ambayo hayajaingiliwa na jeshi lake wakati wa mashambulizi ya ardhini.

Jeshi la Israel laripoti kuweko mashambulizi kutoka Lebanon

Jeshi hilo pia limefahamisha leo kwamba maeneo ya Kiryat Shmona, Biranit na Mount Hermon yaliyo kaskazini mwa Israel, yamelengwa kwa mashambulizi kutoka Lebanon.

Soma pia:Jeshi la Israel lawarai Wapalestina kuondoka Khan Younis

Jeshi hilo limeongeza kuwa kwa kujibu, ndege zake za kivita zimefanya mashambulizi ya kulipiza kisasi katika maeneo yanayoshikiliwa na wanamgambo wenye nguvu wa Hezbollah nchini Lebanon, ikiwa ni pamoja na eneo la kijeshi.

Israel pia imesema imefanya mashambulizi katika eneo yalikotoka mashambulizi hayo ya Lebanon.

Kwa upande wake, vikosi vya usalama vya Lebanon, vimesema kumekuwa na mashambulizi makali kutoka Israel katika vijiji vya Kusini mwa nchi ambavyo haviko mbali na mji wa Kiryat Shmona.