Blinken awasili Cairo kushinikiza amani Mashariki ya kati
18 Septemba 2024Katika ziara yake ya kumi huko Mashariki ya Kati tangu kuanza kwa vita vya Gaza takribani mwaka mmoja uliopita, Blinken atajadili hatua hizo za upatanisho na maafisa wa Misri. Anatarajiwa kukutana na kiongozi wa taifa hilo Abdel Fattah al-Sisi na kufanya mkutano wa pamoja na waandishi habari na mwenzake wa Misri, Badr Abdelatty.
Soma pia:Matumaini ya kusitisha mapigano Gaza yanafifia
Hata hivyo, mara hii Blinken haitoitembelea Israel. Maafisa wa Marekani wanasema hawatarajii mengi makubwa katika mazungumzo yake lakini wanaamini ziara yake itaendelea kuweka shinikizo kwa pande mbili hasimu, Israel na Hamas, kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Ziara yake inafanyika wakati msururu wa vifaa vya mawasiliano vinavyotumiwa na wanachama wa Hezbollah kuripuka katika maeneo kadhaa nchini Lebanon na kusababisha vifo vya watu tisa na kuwajeruhi wengine zaidi ya 2,800 katika shambulizi ambalo Hezbollah inadai limefanywa na Israel.