1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boakai aapishwa kumrithi Weah urais Liberia

22 Januari 2024

Joseph Boakai ameapishwa kuwa rais mpya wa Liberia baada ya kumshinda nyota wa zamani wa kandanda, George Weah, katika uchaguzi wa mwishoni mwa mwaka jana.

https://p.dw.com/p/4bY1e
Joseph Boakai
Rais mpya wa Liberia, Joseph Boakai, ameapishwa kumrithi George Weah.Picha: Carielle Doe/REUTERS

Boakai mwenye umri wa miaka 79 anakabiliwa na changamoto ya kutatua umaskini na ufisadi nchini humo.

Hafla ya kuapishwa Boakai katika majengo ya bunge imehudhuriwa na Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield. 

Rais Boakai atakayeliongoza taifa hilo kwa miaka sita, ana uzoefu wa kisiasa wa miaka 40 na aliwahi kuwa makamu wa rais kati ya mwaka 2006 hadi 2018 chini ya rais wa kwanza mwanamke, Ellen Johnson Sirleaf, kabla ya kushindwa kwa kura nyingi na George Weah katika uchaguzi wa 2017. 

Uchaguzi wa Novemba nchini humo ulikuwa wa amani, katika kanda iliyoshuhudia mapinduzi mfululizo ya kijeshi katika miaka ya karibuni nchini Mali, Burkina Faso, Guinea na Niger.