Bobi Wine awasilisha mahakamani rufaa iliyorekebishwa
9 Februari 2021Hata hivyo, upande wa Rais Museveni umepinga hatua ya kurekebisha shauri hilo ambalo mahakama ya juu inatakiwa kushungulikia na kutoa maamuzi yake kabla ya mwezi Mei ambapo rais mteule anatakiwa kuapishwa.
Kulingana na Medard Lubega Seggona kiongozi wa timu ya mawakili wa Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, wamelazimika kuirekebisha rufaa waliyowasilisha baada ya kutatizwa katika mchakato wao wa kuandaa ushahidi wao wakati mteja wao alipokuwa amewekwa katika kizuizi cha nyumbani.
Hata hivyo Tume ya Uchaguzi ya Uganda pamoja na mawakili wa Rais Museveni wamepinga kurekebishwa kwa rufaa hiyo. Wametoa angalizo kuwa hatua ya upande wa Kyagulanyi kutaka kuongezea ushahidi ili kuonyesha kuwa sheria fulani za uchaguzi zilikiukwa ni suala ambalo hawakubaliani nalo.
Kulingana na ushahidi mpya, upande wa mlalamikaji unahoji hatua ya Tume ya Uchaguzi ya Uganda kutotumia hati za matokeo zilizotoka kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura, matumizi ya teknolojia duni na mashine za kusoma alama za vidole ambazo zilikuwa na hitilafu. Wameitaka mahakama ifahamu kuwa muda wa kurekebisha kesi hiyo ulimalizika kisheria, kama alivyofafanua wakili Ebert Byenkya.
Katika rufaa aliyowasilisha wiki iliyopita, Kyagulanyi aliorodhesha hoja 25 ambazo anataka mahakama izingatie kufutilia mbali kutangazwa kwa Jenerali Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika Januari 14, 2021.
Soma zaidi: Wine kupinga ushindi wa Museveni mahakamani
Miongoni mwa hoja hizo ni hatua ya rais wa sasa kutumia majeshi na raslimali za kitaifa katika kutoa vitisho na kuwashawishi wapiga kura, vitendo vya vyombo vya usalama kumuhangaisha mgombea huyo kuendesha kampeni zake, mienendo ya polisi na jeshi kuharibu na kuchukua picha zake za kampeni, vitendo vya kutekwa nyara na kamatakamata ya wawakilishi wake kwenye vituo vya kupigia kura, kufanyika kwa udanganyifu katika kuhesabu na kutangaza matokeo ya uchaguzi na kadhalika.
Sambamba na hayo, wakaazi katika vituo kadhaa vya kupigia kura wameelezea kushangazwa kuwa kulingana na matokeo ya mwisho ya Tume ya Uchaguzi ya Uganda mgombea huyo Robert Kyagulanyi hakupata kura yoyote katika maeneo ambayo ni ngome yake.
Hadi wakati wa kuandaa taarifa hii mahakama ilikuwa imekwenda kwa mapumziko ili baadaye ifanye maamuzi kama rufaa hiyo irekebishwe.