1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boris Johnson achukua rasmi Mikoba ya Theresa May

24 Julai 2019

Boris Johnson amechukua rasmi nafasi ya kuwa waziri Mkuu nchini Uingereza baada ya Theresa May kujiuzulu.

https://p.dw.com/p/3Mfss
UK Boris Johnson hält Rede vor Downing Street
Picha: Reuters/H. Mckay

Meya huyo wa zamani wa jiji la London aliye na miaka 55 amechukua rasmi Jumatano  nafasi ya Waziri Mkuu punde tu baada ya Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza kumuomba kuunda serikali.

Waziri Mkuu huyo mpya ana miezi mitatu tu ya kutengeneza pale Bi May aliposhindwa na kufanikisha ahadi zake za kuiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ifikapo Oktoba 31.

Boris Johnson tayari ameshamteua Dominic Cummings kama mshauri mkuu wake.

Großbritannien London | Theresa May hält letzte Rede als Premierminsterin in Downing Street
Waziri Mkuu wa zamani Bi Theresa May Picha: Getty Images/AFP/T. Akmen

Alipokuwa anafungasha virago na kuondoka katika ofisi yake ya Downing Street, Bi Theresa May alisema anafurahi kuwa mrithi wake Boris Jonhson ana nia ya kutimiza kile raia wa Uingereza walichokitaka, baada ya kupiga kura ya maoni mwaka 2016 kuondoka katika Umoja wa Ulaya.

Theresa May alisema bado ataendelea na majukumu yake mengine serikalini kama mbunge wa kawaida.

May alitingisha kichwa baada ya kuulizwa na kiongozi wa chama cha upinzani Jeremy Corbyn kama atajiunga nao ili kuzuwiya mipango ya Brexit ya Boris Johnson aliyeahidi kuindoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya ifikapo Oktoba 31 kwa makubaliano au bila makubaliano.

Viongozi kadhaa wajiuzulu kabla ya Boris Johnson kuchukua ofisi ya Waziri Mkuu 

Wakati huo huo, Waziri wa Fedha wa Uingereza, Philip Hammond anayeupinga mpango wa Brexit amejiuzulu muda mchache kabla ya Boris Johnson kuwa waziri Mkuu wa Uingereza.

England, London: Debatte im House of Commons
Waziri wa Fedha Philip Hammond akiwa na Bi Theresa May Picha: Reuters TV

Hammond aliandika katika Ukurasa wake wa Twitter kuwa alimkabidhi rasmi barua ya kujiuzulu kwake Waziri Mkuu wa zamani Theresa May na kumshukuru kufanya nae kazi kwa miaka mitatu.

Wengine waliokataa kufanya kazi na Johnson na kujiuzulu ni Waziri wa Sheria, David Gauke na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa Rory Stewart.

Wote walisema wamejiuzulu kutokana na kutokubaliana na mipango ya Waziri Mkuu mpya juu ya suala la Brexit.

Urusi kwa upande wake kupitia wizara ya kigeni imesema hakuna mabadiliko yoyote katika uhusiano wake na Uingereza kufuatia Johnson kuwa Waziri Mkuu.

Urusi imesema Waziri Mkuu huyo mpya anatokea upande wa wale waliyoyaharibu mahusiano ya nchi hizo mbili.

Vyanzo: Reuters/dpa/afp