1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boris Johnson: Uingereza kuondoaka Umoja wa Ulaya Oktoba 31

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
25 Julai 2019

Waziri mkuu mpya wa Uingereza Boris Johnson ameahidi kuifanya Uingereza kuwa nchi ya neema kuliko nchi yoyote duniani na amesisitiza msimamo wake wa kwamba nchi hiyo itatoka kwenye Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/3MjXj
Großbritannien London | Neuer Premierminister Boris Johnson spricht im britischen Unterhaus
Picha: Reuters TV

Waziri Mkuu Boris Johnson amesema jukumu la serikali yake ni kuiondoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya  tarehe 31 mwezi Oktoba ili kuwaleta waingereza wote pamoja na kuiimarisha nchi. Waziri Mkuu huyo mpya ameahidi kufikia mapatano mapya na Umoja wa Ulaya katika muda usiozidi siku 99 lakini ameonya kwamba, ikiwa viongozi wa Umoja wa Ulaya watakataa, basi Uingereza itajiondoa bila ya mkataba. Hata hivyo amesema anaamini kuwa uwezakano wa Umoja wa Ulaya kukataa mkataba mpya ni mdogo sana. Johnson amesema masharti yaliyomo kwenye mkataba wa sasa hayakubaliki.

Johnson amesema Mkataba juu ya Uingrezea kujiondoa Umoja wa Ulaya uliojadiliwa na waziri mkuu wa hapo awali ulikataliwa mara tatu. Masharti yake hayakubaliki kwa bunge na kwa nchi ya Uingereza. aliwaambia wabunge kwamba nchi yoyote inayothamini uhuru wake na hadhi yake haiwezi kuukubali mkataba kama huo wa kutosa uhuru wa kiuchumi na kwamba hakuna anayeweza kuukubali mkataba kama huo unaohusu mpaka wa Ireland.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Getty Images/AFP/T. Akmen

Akihutubia bungeni kwa mara ya kwanza kama waziri mkuu bwana Johnson amesema kipengele kinachohusu mpaka wa Ireland kinapaswa kuondolewa kabisa kwenye mkataba wa Brexit. Amesema, inapaswa ieleweke wazi kwamba njia ya kufikia mapatano ni kuliondoa suala la mpaka wa Ireland. 

Bwana Johnson anatumai kufanikiwa kuyashawishi mataifa makubwa ya Ulaya, Ujerumani na Ufaransa  yakubali mazungumzo mapya, kwa kutumia kitisho cha kujiondoa Uingereza Umoja wa Ulaya bila ya mkataba. Lakini Umoja wa Ulaya umeshatoa jibu.

Msemaji wa jumuiya hiyo ameeleza kwamba Umoja wa Ulaya hautaanzisha mazungumzo mapya juu ya Brexit kwa ajili ya suala la mpaka wa Ireland licha ya Waziri Mkuu Boris Johnson kusisitiza kwamba atadai mabadiliko katika mkataba wa sasa.

Msemaji huyo, Mina Andreeva ameeleza kuwa  Umoja  wa Ulaya uko tayari kuzungumzia nyongeza katika  tamko la kisiasa juu ya uhusiano wa baadae kati yake na Uingereza lakini hauko tayari kuuzungumzia mkataba uliopo.

Katika kadhia nyingine  Waziri  Mkuu wa Uingereza wa hapo awali Theresa May leo aliamua kwenda  kuangalia mechi ya mchezo wa Cricket kati ya Uingereza na Ireland badala ya kwenda bungeni kuisikiliza hotuba ya Waziri Mkuu mpya Boris Johnson.

Vyanzo:/ DPAE/APE/RTRE/AP/DPA