Boris Johnson ziarani Belfast kuhusu mzozo wa Brexit
16 Mei 2022Katika tukio la kihistoria, nafasi ya waziri wa kwanza wa Ireland ya Kaskazini inatarajiwa kuchukuliwa na chama cha Sinn Fein kinachoiunga mkono Jamhuri ya Ireland, baada ya kushinda uchaguzi wa bunge la Stormont mapema mwezi huu
Lakini chama cha Democratic Unionist (DUP) kinachounga mkono Uingereza, ambacho kilighadhabishwa na itifaki ya Ireland Kaskazini, iliyokubaliwa kama sehemu ya makubaliano ya Brexit na Umoja wa Ulaya, kilizuia uchaguzi wa spika katika bunge hilo la Stormont.
Johnson atakutana na vyama husika na anatarajiwa kuwaambia kwamba London itatekeleza wajibu wake kuhakikisha utulivu wa kisiasa. Lakini sharti wanasiasa wa Ireland ya Kaskazini warejee kazini kushughulikia masuala muhimu. Hayo ni kulingana na taarifa kutoka ofisi ya Johnson.
Mvutano wa uundwaji uongozi Ireland Kaskazini
Chama cha DUP kimekataa kusaidia uundwaji wa uongozi hadi pale itifaki hiyo itakapobadilishwa na kuondoa ukaguzi wa kibiashara kati ya Ireland Kaskazini na Uingereza, ambao kinaamini unatishia hadhi ya jimbo hilo ndani ya Uingereza.
Ulaya yawasilisha mapendekezo kuepusha mzozo mpya wa Brexit
Serikali ya Johnson pia inasisitiza kuwa itifaki hiyo inatishia usawa wa amani katika Ireland ya Kaskazini kati ya jumuiya ya wazalendo wanaotaka kujiunga na Jamhuri ya Ireland, na wale wanaopendelea kuendelea kuwa sehemu muungano na Uingereza.
Imeonya kuwa itaanzisha kifungu cha 16 cha mkataba wa Brexit kusitisha makubaliano hayo, au kutunga sheria ya kuondoa masharti yake kwenye sheria za Uingereza, isipokuwa tu kama Umoja wa Ulaya utakubalia kuyabadilisha.
Ukaguzi wa bidhaa kutoka England, Scotland na Wales
Utaratibu huo umeweka masharti kwa bidhaa zinazoingizwa katika jimbo hilo kutoka England, Scotland na Wales, ili kuhakikisha hakuna kurudishwa kwa mpaka kati ya Ireland Kaskazini na Ireland ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya.
Biden, Johnson wakutana kwa mkataba mpya
Ziara ya Johnson inatarajiwa kufanyika wakati sawa na ujumbe wa bunge la Marekani. Marekani ndiyo ilibeba dhamana ya mkataba wa Good Friday na imeelezea hofu yake kuhusu vitisho vya Uingereza dhidi ya utaratibu huo.
Mnamo Ijumaa wiki iliyopita, msemaji wa Johnson aliwaambia waandishi wa habari kwamba hali imekuwa tete Zaidi n ani lazima Umoja wa Ulaya iweze kubadili msimamo. Lakini umoja huo umeshikilia kwamba makubaliano ya Brexit hayawezi kujadiliwa upya.
(Afpe)