Borussia Dortmund bado kidume
21 Septemba 2015Borussia Dortmund imerejea kileleni mwa ligi jana Jumapili baada ya kuikandika Bayer Leverkusen kwa mabao 3-0 na kuendeleza rekodi yao ya kutofungwa hadi sasa katika msimu huu wa bundesliga.
Dortmund imeshinda michezo 11 katika mashindano mbali mbali msimu huu , lakini wanaongoza Bundesliga kwa kuwa na wingi tu wa magoli kutoka kwa mabingwa watetezi Bayern Munich , ambao nao wameshinda michezo yao yote mitano baada ya kuishinda Darmstadt kwa mabao 3-0 siku ya Jumamosi.
Mchezaji wa Damstadt Marcel Heller amesema hakuna ubishi Bayern si rahisi kupambana nayo.
"Leo dhidi ya Bayern ilikuwa wazi , tulicheza dhidi ya timu ngumu kabisa duniani, kupambana nayo ilikuwa vigumu sana. Tuliona, vipi waliweza kuudhibiti mpira, na vipi waliweza kutafuta njia ya kupata nafasi ya kufunga mabao. Na hatupaswi kudondosha chozi, kwa kuwa tumeshindwa leo."
Hata hivyo kutokana na jinsi Dortmund inavyocheza kuna kila sababu kwamba mbio za kuwania ubingwa msimu huu nchini Ujerumani zitakuwa za kuvutia baada ya Bayern kushinda Bundesliga katika misimu mitatu iliyopita bila kupata upinzani wa maana .
Augsburg imepata ushindi wake wa kwanza katika msimu huu kwa kuibwaga Hannover 96 kwa mabao 2-0 jana Jumapili , ambapo hapo kabla Schalke 04 ilisababisha machungu zaidi kwa VFB Stuttgart baada ya kuizamisha kwa bao 1-0. Stuttgart bado inasaka ushindi wake wa kwanza msimu huu baada ya michezo mitano, ikiwa na pointi moja tu kibindoni. Kocha wa Schalke Andre Breitenreiter hata hivyo amekiri kuwa ushindi huo ulikuwa wa bahati.
"Leo ilikuwa ushindi wa bahati . Kwa ushindi wetu tunapaswa kwanza kumshukuru mlinda mpango wetu Ralf Fährmann, ameonesha uwezo wa hali ya juu kabisa. Stuttgart ilikuwa tangu mwanzo wa mchezo wakipambana na wakikimbia huku na huko,wakicheza vizuri sana. Hawakucheza kabisa kama timu ambayo haijapata pointi hadi sasa. Iwapo wangetumia vizuri nafasi walizopata , basi wangekuwa na mafanikio makubwa."
Msimu wenye mashaka makubwa umeizukia pia Borussia Moenchengladbach , baada ya Jumamosi kuonja tena chungu ilipokubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya majirani zao FC Kolon , katika mchezo wa watani wa jadi wa eneo la Rhineland na kujikita zaidi mkiani mwa ligi.
Hatua hiyo ya FC Kolon kutoonyesha ujirani mwema kwa jirani mwenye matatizo imesababisha kocha wa Gladbach ucien Favre kujiuzulu akisema haoni kwamba anastahili kuwa kocha wa timu hiyo ambayo imekwisha tawazwa mabingwa wa Bundesliga mara tano katika miaka ya 1970. Hata hivyo uongozi wa klabu hiyo bado haujakubali kujizulu kwake. Gladbach inakabiliwa na michezo miwili ya ligi wiki hii ikiwa nyumbani dhidi ya Augsburg siku ya Jumatano na ugenini inapambana na Stuttgart timu nyingine iliyomo katika matatizo makubwa msimu huu.
Mkurugenzi wa spoti wa Gladbach Max Eberl amesema wanajaribu kumshawishi Favre kuendelea na kibarua hicho wakati kikosi hicho kinaikabili Manchester City katika siku kumi zijazo katika Champions League, na kisha itakabiliana na makamu bingwa wa Bundesliga VFL Wolfsburg.
"Tunaamini kwa dhati kwamba Lucien Favre ndio kocha sahihi kwa Borussia na tutaweza kutoka kutoka katika hali hii mbaya pamoja , amesema Eberl katika taarifa. Kocha wa FC Kolon timu iliyovuruga kabisa mwelekeo wa Gladbach siku ya Jumamosi Peter Stöger amesema ilikuwa muhimu kushinda mchezo huo.
"Ni muhimu, kwamba kwa mara nyingine tena tumeshinda. Ni muhimu, kwasababu pointi kwetu ni muhimu. Hali hiyo inatupa kidogo nafasi ya kupumua na kujikuta katika hali salama kidogo, na hii inaleta utulivu katika kikosi. Pia inatoa fursa kwa nyakati za matatizo kukubali kwamba umefungwa na maisha yanaendelea."
Bundesliga yarejea tena uwanjani
Bayern Munich lakini inarejea tena uwanjani kesho Jumanne ikipambana na makamu bingwa VFL Wolfsburg ikiwania kuwa timu ya kwanza kushinda mataji manne mfululizo katika Bundesliga. Wolfsburg , mabingwa wa kombe la shirikisho DFB Pokal , imeshaifunga Bayern msimu huu baada ya kushinda katika kombe la ufunguzi wa msimu Super Cup kwa mikwaju ya penalti.
Borussia Moenchengladbach inakwaana na Augsburg , siku ya Jumatano ikitafuta pointi yake ya kwanza msimu huu. Borussia Dortmund ikiwa upande wa pili wa msimamo wa ligi iko nyumbani kwa Hoffenheim siku ya jumatano ikisaka ushindi wake wa sita katika Bundesliga mfululizo msimu huu.
Hertha Berlin inapambana na FC Kolon kesho Jumanne, Ingolstadt inaikaribisha Hamburg SV, Darmstadt nayo iko nyumbani ikiisubiri Werder Bremen.
Jumatano ni Schalke ikiumana na Eintracht Frankfurt , Mainz 05 inasafiri kwenda kwa Bayer Leverkusen, na Hannover 96 inatiana kifuani na VFB Stuttgart.
Manchester City yaonja joto la jiwe
Katika premier League nchini Uingereza , viongozi wa ligi hiyo msimu huu Manchester City imekubali kipigo cha kushitukiza cha mabao 2-1 nyumbani dhidi ya West Ham United na kumaliza rekodi yake ya asilimia 100 ya ushindi na kupunguza uongozi wake hadi pointi mbili kwa mahasimu wake Manchester United.
Chelsea iliizamisha Arsenal kwa mabao 2-0 katika mchezo wa watani wa jadi uliojaa vituko na mijadala kuhusiana na wachezaji , maoni ya makocha na pia maswali kadhaa juu ya mwamuzi wa mchezo huo. Arsenal ilimaliza mchezo huo ikiwa na wachezaji tisa uwanjani.
La Liga
Lionel Messi alipachika mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Levante katika ligi ya Uhispania La Liga.
Goli la karim Benzema lilitosha kuivusha Real madrid katika patashika dhidi ya Granada ambao walikasirishwa na kukataliwa kwa bao la mshambuliaji wake Youssef El-Arabi.
Barcelona inaingia tena uwanjani siku ya Jumatano kupambana na Celta Vigo , na siku hiyo pia kutakuwa na pambano kati ya Sevilla ikipambana na Las Palmas. Levante itapambana na eibar, Malaga inaikaribisha Villareal.Kesho Jumanne , Atletico Madrid inaikaribisha Getafe na Real Sociedad inakwenda nyumbani kwa Granada.
Nchini Italia , Inter Milan imeendeleza ushindi wake baada ya kubandika Chievo bao 1-0 na kuiweka timu hiyo kuwa pekee yenye pointi 12 kutokana na michezo 4 ya mwanzo.
Torino iko nafasi ya pili baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Sampdoria Genoa.
Mabingwa Juventus wamepata ushindi wao wa kwanza msimu huu baada ya kuishinda Genoa kwa mabao 2-0.
Paris St. Germain imeshindwa mara mbili kupata ushindi baada ya kutoshana sare na Stade de Reims kwa kufungana bao 1-1 lakini imeendelea kuongoza ligi hiyo.
Matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu , Doping.
Shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA amepuuzia dhana kwamba matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu misuli huenda ni kitu cha kawaida miongoni mwa wachezaji kandanda baada ya utafiti ulioidhinishwa na shirikisho hilo kuonesha idadi kubwa ya viwango vya madawa hayo.
Utafiti huo , ambao umechapishwa katika jarida la kila mwezi la sayansi mwezi huu, umesema viwango vya juu vya madawa vimeonekana katika sampuli za mkojo za asilimia 7.7 ya wachezaji 879 waliofanyiwa uchunguzi na watafiti. Viwango hivyo vinaonesha matumizi ya madawa kama hayo ya kuongeza nguvu misuli.
UEFA haikutangaza utafiti huo , ambao umepatikana jana Jumapili katika ripoti iliyotolewa na kituo cha televisheni cha Ujerumani ARD, lakini imetangazwa mwezi huu kwamba matumizi ya steroid kwa wachezaji yanaongezwa katika mpango wake wa kibaolojia.
UEFA imesema ina mpango wa kina wa kupambana na matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu mwilini kwa miaka mingi kwa kufanya zaidi ya majaribio ya uchunguzi 2,000 kwa mwaka na ni wawili tu wamepatikana na hatia ya kutumia madawa hayo.
Mbio za magari ya Formula one
Sebastian Vettel ameshinda mbio za magari za Formula one katika Singapore Grand Prix, hali inayofanya mashindano hayo msimu huu kuwa ya kuvutia. Lakini viongozi wa mashindano hayo Mercedes wana imani kwamba watarejea tena kileleni kutoka mwisho wa wiki ya kukatisha tamaa, kwa Lewis Hamilton kushindwa kumaliza mbio hizo na kujitoa kwa mara ya kwanza msimu huu.
Dereva mwingine wa Mercedes Nico Rosberg alishindwa pia hata kuchukua nafasi ya nne.
Na kwa taarifa hiyo ndio tunafikia mwisho wa kuwa nawe katika ukurasa huu wa michezo jioni ya leo. Jina langu ni Sekione Kitojo , hadi mara nyingine kwaherini.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / ape / afpe / rtre
Mhariri :M0ohammed Abdul-Rahman