1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Borussia Dortmund yaanza kwa kishindo

Admin.WagnerD24 Agosti 2015

Borussia Dortmund yaanza kwa kishindo msimu huu , ikishikilia usukani wa ligi hiyo, Bayern yaendeleza nia yake kunyakua kunyakua ubingwa mara ya nne.

https://p.dw.com/p/1GKni
Bundesliga FC Ingolstadt gegen Borussia Dortmund
Picha: L. Preiss/Bongarts/Getty Images

Borussia Dortmund imepanda kileleni mwa msimamo wa ligi ya Ujerumani jana Jumapili baada ya kuirarua Ingolstadt kwa mabao 4-0 , dozi iliyotoa kwa Borussia Moenchengladbach wiki iliyopita katika mchezo wa ufunguzi .

Msimu uliopita Borussia Dortmund ilikuwa inasua sua baada ya kupata vipigo mfululizo , na hatimaye kuamua kuachana na kocha wake mahiri Juergen Klopp ambaye ameipa timu hiyo uwezo mkubwa na kuwa moja kati ya timu zinazoogopwa katika bara la Ulaya.

Mathias Ginter na Marco Reus walipata mabao ya mwanzo kwa timu hiyo kabla ya Shinji Kagawa na Pierre-Emerick Aubameyang kuongeza mabao mawili na kuiweka Dortmund kileleni mwa ligi ya Bundesliga mara ya mwisho katika nafasi hiyo ikiwa ni Septemba mwaka 2013. Kocha wa Borussia Dortmund Thomas Tuchel amesema haangalii kwa sasa nani yuko juu ama chini.

Fußball Bundesliga FC Ingolstadt - Borussia Dortmund
Matthias Ginter baada ya kufunga bao la kwanza la Borussia DortmundPicha: Getty Images/AFP/C. Stache

"Kwasasa tunajiangalia sisi zaidi. Mtazamo wetu ni juu ya nini tunakihitaji zaidi, kipimo chetu kiko wapi, na kwa hilo najisikia vizuri sana."

Nae kocha wa timu iliyopanda daraja msimu huu Ingolstadt Ralph Hasenhüttl amesema tulifanya vizuri lakini si vizuri vya kutosha. "Kwa kipindi kirefu tulifanya vizuri sana. Tulijaribu , kupambana kiume na mpinzani wetu na kuwashughulisha. Lakini wana uwezo mkubwa sana , kwa hiyo ilikuwa vigumu kwetu. Lakini nimefarijika licha ya ugumu huo kwa timu yangu. Kile walichokifanya katika muda wa dakika 90 , ni kazi nzuri sana. Ni kwa njia hiyo tu tutaweza kupata mafanikio."

Kwa upande wake Borussia Moenchengladbach imeanza msimu huu vibaya, baada ya kupata kipigo mara mbili, ambapo jana iliangushwa na Mainz 05 kwa mabao 2-1.

Mchezaji wa kati wa Moenchengladbach Patrick Herrmann amekiri kwamba timu yake ilishindwa kufunga mabao baada ya kupata nafasi za wazi.

"Tulipata nadhani nafasi tau , ama nne za wazi kabisa kuweza kupata bao leo, na ilikuwa ni lazima tupate bao moja ama mawili na mchezo huo ungekuwa tofauti kabisa. Lakini tumeshindwa wenyewe kufikisha mwisho."

Fußball Bundesliga Borussia Mönchengladbach gegen FSV Mainz 05
Wachezaji wa Mochengladbach wakipambana na Mainz 05Picha: Getty Images/AFP/P. Stollarz

Kwa upande wa washindi Mainz 05 ambao katika mchezo wa kwanza wa Bundesliga waliambulia kipigo kutoka kwa Damstadt cha bao 1-0 wiki iliyopita , mchezaji wa mainz Fabian Frei anasema zilikuwa pointi tatu muhimu.

"Pointi tatu ni muhimu sana, kwa ajili ya kujenga morali. Nafikiri hatukupata maandalizi mazuri kuelekea katika ligi. Kwa hiyo tukapata kipigo wiki iliyopita. Na kwa sasa tunajisikia vizuri sana, kwamba tunafurahia ushindi kama huu."

Bayern Munich ilihitaji nguvu ya ziada kuweza kuwaangusha Hoffenheim nyumbani kwao kwa mabao 2-1 kwa bao la Robert Lewandowski baada ya kuwa nyuma kwa bao moja kwa muda mrefu , ambapo wenyeji walijipatia bao lao sekunde tisa baada ya mchezo kuanza kupitia mshambuliaji Kevin Volland.

Bayer Leverkusen nayo imejiunga na Dortmund na Bayern katika pointi 6 , baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Hannover 96.

Bayern Munich hawana mpango ya kusajili mchezaji wa kati wa VFL wolfsburg Kevin De Bruyne, mchezaji anayewindwa sna na Manchester City , licha ya taarifa zinazoelekeza kwamba wanaweza kufanya juhudi za kumpata, klabu hiyo imesema leo Jumatatu. mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 kutoka ubelgiji , ambaye mkataba wake unamalizika 2019, amehusishwa na kuhamia Man City wakati mkurugenzi wa spoti wa Wolfsburg Klaus Allofs akithibitisha kwamba klabu hiyo ya premier league imeonyesha kumhitaji mara kwa mara.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman