Borussia Dortmund yaendelea kuporomoka
6 Oktoba 2014Borussia Moenchengladbach walitoka uwanja janaJumapili (05.10.2014) wakiwa hawakuridhika na matokeo ya pambano lao dhidi ya FSV Mainz 05, baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa mwisho wa duru ya saba ya Bundesliga. Gladbach imeshindwa kuchupa na kuwakaribia viongozi wa ligi hiyo na mabingwa watetezi Bayern Munich . Gladbach ilikuwa inatarajia kufika katika nafasi ya pili, ambayo hivi sasa inashikiliwa na 1899 Hoffenheim.
Hoffenheim inashikilia nafasi hiyo baada ya kuipiga mwereka Schalke 04 kwa mabao 2-1 siku ya Jumamosi , ambapo mshambuliaji wa timu hiyo Kevin Volland amesema wamecheza mchezo wao bora kabisa katika msimu huu hadi sasa.
"Leo tumecheza mchezo wetu mzuri zaidi katika msimu huu. Upande wa ulinzi ulikuwa imara, katika kila hali, na hatukutoa nafasi nyingi za kutuvuruga na upande wa ushambuliaji tulishambulia vizuri kwa kushitukiza. Tungeweza pia kupata mabao mengi zaidi. Pamoja na hayo tumeweza kucheza vizuri wakati wote."
Katika mchezo wa kwanza jana Wolfsburg ilipata ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Augsburg.
Dortmund hoi
Na katika michezo mingine siku ya Jumamosi, Borussia Dortmund ambayo imeanza msimu huu ikiwa na majeruhi kadhaa , imeshindwa tena kutamba mbele ya Hamburg SV, timu ambayo ilikuwa ikiwania kupata ushindi wake wa kwanza msimu huu. Hamburg iliipiga mwereka Dortmund nyumbani kwa bao 1-0 ushindi wa kwanza wa Hamburg msimu huu na kipigo ambacho Dortmund haitakisahau , kwani kimeitumbukiza timu hiyo katika hali ya wasi wasi mkubwa.
Mshambuliaji wa Hamburg SV ambaye ndie aliyefunga bao hilo Pierre-Michel Lasogga amesema kila mmoja amefahamu kuwa juhudi zetu katika michezo iliyopita hazitapita bure.
"Naamini, katika michezo yetu mitatu iliyopita tulionesha, tunaelekea wapi. Dhidi ya FC Bayern tulicheza vizuri, dhidi ya Gladbach na Frankfurt pia. Tulipata bahati mbaya kidogo katika michezo miwili. Leo baada ya juhudi zetu tumefanikiwa. Hadi dakika ya mwisho tulipambana na ndio sababu naweza kusema, timu ilicheza vizuri, na ushindi mzuri."
Bayern Munich imeonesha kuwa bado ni moto wa kuotea kwa mbali baada ya kuirarua Hannover 96 kwa mabao 4-0, na ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 17, tayari inatayarisha sherehe za ubingwa wa mapema huenda Februari mwakani.
TSG Hoffenheim inafuatia ikiwa na pointi 13 sawa na Borussia Moenchengladbach ambayo pia ina pointi 13.
Ronaldo hashikiki katika La Liga
Na huko nchini Uhispania , viongozi wa ligi ya nchi hiyo La Liga , Barcelona imekuwa timu ya kwanza kucheza michezo saba bila ya kufungwa bao mwanzoni mwa msimu wakati Lionel Messi na Neymar walipofunga mabao katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Rayo Vallecano siku ya Jumamosi.
Mabingwa Atletico Madrid walikwaa kisiki na kukubali kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya valencia, ambayo imejiimarisha katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 17, mbili nyuma ya Barca.
Cristiano Ronaldo ameendelea kuzitembelea nyavu za timu pinzani kama anavyotaka baada ya kufunga mabao 3 jana wakati Real Madrid ikiirarua Athletic Bilbao kwa mabao 5-0 jana Jumapili na kupanda hadi nafasi ya nne kwa mara ya kwanza msimu huu.
Juventus Turin ya Italia iliishinda AS Roma kwa mabao 3-2 katika mchezo wa ligi ya Italia Serie A, wakati timu hizo mbili zilizoko kileleni mwa ligi hizo zilipombana jana Jumapili.
Mabingwa wa Ufaransa Paris Saint German waliridhika na sare ya bao 1-1 dhidi ya makamu bingwa Monaco uwanjani Parc des Princes.
Chelsea imeendelea kupata ushindi na kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi ya Uingereza Premier League na kufungua mwanya wa pointi tano kwa kuishinda Arsenal kwa mabao 2-0 jana Jumapili.
Mourinho na Wenger wavutana mashati
Hata hivyo pambano hilo la watani wa jadi lilikuwa na matukio ambayo si ya kawaida, ambapo makocha wa timu hizo ilibidi kuonywa na mwamuzi baada ya kusukumana kutokana na tukio la uwanjani.
Kocha wa Arsenal , Aserne Wenger alimsukuma ,kocha wa Chelsea Jose Mourinho katika pambano hilo lenye hamasa nyingi.
Je tukio hilo linaweza kusababisha kufungiwa kwa muda kwa kocha wa Arsenal Wenger ambaye alimsukuma Mourinho wa Chelsea?
Mvutano wa muda mrefu kati ya Arsene Wenger na Jose Mourinho hauonekani kutoa ishara ya kupata nafuu. Lakini kocha wa Chelsea Jose Mourinho amewaambia wachezaji wake wasijisikie kichwa kikubwa baada ya ushindi huo wa mabao 2-0 dhidi ya Arsenal.
Na katika mpira wa kikapu:
Timu ya Marekani ya wanawake ya mpira wa kikapu imepata ushindi dhidi ya Uhispania kwa ushindi wa mabao 77-64 na kunyakua taji la ubingwa wa dunia kwa mara ya pili mfululizo jana(05.10.2014) mjini Istanbul Uturuki.
Na katika mchezo wa tennis , Maria Sharapova amepanda hadi nafasi ya pili katika orodha ya shirikisho la mchezo huo duniani WTA nyuma ya Serena Williams, siku moja baada ya kumshinda Petra Kvitova kwa seti 2-1 , 6-4 , 2-6, na 6-3 katika mashindano ya China Open.
Kwa upande wa wanaume Novak Djokovic ameendelea kubaki kileleni , akifuatiwa na rafael Nadal na Rodger Federer wa Uswisi katika nafasi ya tatu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / afpe / rtre / dpa
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman