Borussia Dortmund yakosa mwelekeo
30 Oktoba 2017Tukianza na Bundesliga, Borussia Dortmund imetumbukia katika hali ya sintofahamu baada ya kushindwa kupata matokeo mazuri katika michezo mitatu ya ligi ambapo imeambulia pointi moja tu na kufungwa takriban mabao 9 na kuweka wazi udhaifu wa safu ya ulinzi ya timu hiyo. borussia Dortmund imeshindwa mwishoni mwa wiki kutetea uongozi wake wa ligi na kukubali kipigo cha mbwa mwizi baada ya kukandikwa mabao 4-2 na timu iliyopanda daraja msimu huu Hannover 96 kipigo kilicholeta gumzo kubwa kuhusu kocha mkuu Peter Bosz kwamba hana plan B wakati timu ikiwa imekwama katika mpango wa kwanza. Mlinda mlango wa Borussia Dortmund anatathmini kuhusu mchezo ulivyokuwa.
"Tulijua , kwamba ni timu nzuri. wanafanyakazi kama timu, na leo wameonesha hivyo. Wana wachezaji , wawili ama watatu , ambao wanafanyakazi vizuri sana. Hatukuweza kabisa kufanya vizuri upande wa ulinzi. Tulishindwa kabisa mapambano ya mtu na mtu. Hii nazungumzia pamoja na mimi binafsi. Bila shaka utapata kipigo unapokutana na timu nzuri."
Borussia Bortmund hivi sasa inashika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa watetezi Bayern Munich. Bayern hivi sasa ina pointi 23 tatu zaidi ya Borussia Dortmund baada ya kuiandika RB Leipzig kwa mabao 2-0 katika mchezo mwingine uliokuwa na mivutano kadhaa na maamuzi ya kutatanisha. RB Leipzig inabakia katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 19.
Hannover baada ya kuangusha mbuyu siku ya Jumamosi dhidi ya Borussia Dortmund sasa imepanda hadi nafasi ya nne ikiwa na pointi 18 , FC Schalke 04 imeingia katika nafasi ya juu kwa mara ya kwanza katika kipindi cha misimu miwili ikiwa katika nafasi ya tano baada ya kutoka sare na Wolfsburg kwa kufungana bao 1-1.
FC Kolon bado inagagaa katika nafasi ya mkiani mwa ligi ya Ujerumani baada ya kupokea nayo kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya watani wao wa jadi Bayer 04 Leverkusen. Wakati Leverkusen imesogea nafasi moja kutoka ya tisa hadi ya nane ikiwa na pointi 15 , FC Kolon imebakia na pointi 2 tu kibindoni.
Kocha Nagelsmann akasirishwa na kipigo
Baada ya kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Borussia Moenchengladbach, kocha wa Hoffenheim alikasirishwa sana na timu yake inavyocheza na kutupa chupa ya maji ambayo iliangukia kwa mashabiki na hatimaye kutakiwa na refa kwenda kuangalia kandanda akiwa na mashabiki badala ya benchi la ufundi.
"Nashukuru Mungu kwamba haikumpata mtu, badala yake iligonga ukutani. Iliporudi chupa ilimgonga shabiki. Na ndipo nilipoamriwa kwenda kukaa jukwaani na naomba radhi kwa kitendo hicho. samahani sana, kutokana na kitendo changu cha kijinga, ambacho hakikupaswa kutokea na sitafanya tena. Nilimkumbatia, na hata kama angekuwa shabiki wa Gladbach ningemkumbatia. Isingekuwa rahisi lakini ningejaribu."
Werder Bremen ilikandikwa mabao 3-0 na Augsburg na kubakia katika nafasi ya 17 ikiwa na pointi 5 tu katika michezo 10 . Ndio sababu leo hii timu hiyo imetengana rasmi na kocha wake mkuu Alexander Nouri . Klabu hiyo kutoka kaskazini mwa Ujerumani imethibitisha leo Jumatatu chini ya masaa 24 baada ya kubungizwa mabao 3-0 na Augsburg nyumbani.
Nouri aliteuliwa msimu uliopita na kuiongoza klabu hiyo kuepuka kushuka daraja na kukaribia kuingia katika nafasi za kucheza kombe la ligi ya Ulaya. Lakini sare tano na kichapo mara tano vimemgharimu kocha Nouri kibarua chake. Mshambuliaji wa Werder Bremen na nahodha wa timu hiyo Zlatko Junuzovic anasema.
"Matokeo ni mabaya, hali ni mbaya. Hatuwezi hivi sasa kulalamikia hali hii au lolote lile. Tumejiingiza wenyewe katika hali hii. Wenyewe ndio tunamakosa na lazima tujitoe. Sijui , ni vipi au nini kinakuja, lakini hatimaye , bila kujali nini kimetokea, kama timu inatubidi kusimama pamoja na kuonesha uwezo wetu uwanjani."
Kocha msaidizi
Werder Bremen imesema kocha wake wa timu ya vijana wa chini ya miaka 23 Florian Kohfeldt , pamoja na kocha msaidizi Thomas Horsch wa kikosi cha vijana wa chini ya miaka 17 na kocha msaidizi wake Tim Borowski wataitayarisha timu hiyo kwa ajili ya pambano la ligi hapo Ijumaa ikiifuata Eintracht Frankfurt.
Katika kombe la shirikisho nchini Ujerumani maarufu kama DFB Pokal , hivi sasa likiingia katika duru ya robo fainali, Bayern Munich ambayo imelinyakua kombe hilo mara nyingi zaidi inawasubiri katika duru yaq timu 16 zilizobakia Borussia dortmund mabingwa watetezi wa kombe hilo.
Timu hizo za juu katika Bundesliga kwa sasa zimepambana katika fainali mwaka 2012, 2014 na 2016. Katika misimu iliyopita vilabu hivyo zimekutana katika nusu fainali, na BVB ilishinda mpambano huo kwa mabao 3-2 mjini Munich msimu uliopita na hatimaye kunyakua ubingwa dhidi ya Frankfurt.
Frankfurt iliyofikia fainali msimu uliopita itakwaana na FC Heidenheim ya daraja la pili. SC Paderbon ambayo ni timu pekee ya daraja la tatu iliyobakia katika kinyang'anyiro hicho , inaisubiri FC Ingolstadt ya daraja la pili. Michezo hiyo ya robo fainali inatarajiwa kufanyika kati ya tarehe 19 na 20 mwezi Desemba.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre / afpe / ape
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahaman