Borussia Moenchengladbach yajizatiti kileleni mwa Bundesliga
2 Desemba 2019Viongozi wa ligi Borussia Moenchengladbach tayari wameonesha mshangao wa kupanda hadi kileleni mwa msimamo wa ligi kuwa si kwa bahati mbaya na ushindi wao jana wa mabao 4-2 dhidi ya Freiburg inaleta mvuto katika pambano la siku ya Jumamosi dhidi ya mabingwa watetezi Bayern Munich , ambayo siku ya Jumamosi ilichezea kipigo cha mabo 2-1 dhidi ya Bayer Leverkusen nyumbani. Gladbach , ambayo imeshinda michezo minane katika michezo yao 10 iliyopita, imefungua mwanya wa pointi 4 mbele ya Bayern Munich iliyoko katika nafasi ya 4 na wanashika usukani wa ligi kwa wiki ya saba mfululizo, ikiwa ni mwendo wao bora kabisa tangu msimu wa mwaka 1977 ambapo walinyakua taji hilo la Bundesliga.
Huyu hapa mlinzi wa Bayern Munich Joshua Kimmich akizungumzia kipigo cha kwanza tangu timu hiyo kumtimua kocha wake mkuu Niko Kovac ilipokutana na dhidi ya Gladbach siku ya Jumamosi jioni.
"Idadi kubwa ya nafasi za kupata mabao ilikuwa kwetu, tangu wakati ambao naweza kuukumbuka, hakuna wakati tulikuwa na nafasi kama hizo kupata mabao. Pia tumekuwa katika hali ya kuotea mara mbili au tatu, lakini pamoja na hayo, takriban tulistahili kuwa sare ya 2-2 tukienda mapumziko. Na hata baada ya kuanza kipindi cha pili tulipata pia nafasi mbili ama tatu za kupata mabao."
Baada ya kushinda mara nne bila nyavu zao kutikiswa chini ya kocha wa mpito Hansi Flick, Bayern ilirejeshwa kutoka uwingu wa juu kwa kipigo hicho, nyumbani dhidi ya Leverkusen.
Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani Juergen Klinsmann amerejea katika ukufunzi wa timu za Bundesliga baada ya kuondoka muongo mmoja uliopita lakini kazi hiyo akiwa na Hertha Berlin ilitiwa doa na kipigo cha mabao 2-1 nyumbani dhidi ya makamu bingwa wa Bundesliga Borussia Dortmund. "Tulihitaji zaidi kidogo. Hatutaongeza nguvu zaidi," amesema Klinsmann, ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya klabu hiyo.
"Walikuwa wamejikusanya mno nyuma na kimsingi walipaki basi, na kuweza kupenya kuelekea golini, unahitaji washambuliaji watano. Hii ni vigumu sana. Lakini jinsi timu ilivyocheza, kujituma, kama walivyokuwa wakisaidiana, pia kukimbia sana na mapambano ya mtu na mtu, ilikuwa vizuri sana. Kutokana na hayo tunapaswa kujenga , na tumefanya hivyo kwa kazi kubwa na kujenga tabaka la mafanikio, ambalo hatimaye pointi zitakuja."
Kocha wa Borussia Dortmund ambaye amekabiliwa na ukosoaji mkubwa wa kikosi chake kukosa msisimko uwanjani , amepumua kidogo kutokana na ushindi huo, baada ya vipigo na sare ambazo zilisababisha mashabiki na wachambuzi wa masuala ya kandanda nchini Ujerumani kutak viongozi wa klabu hiyo wamtimue kocha huyo Mswisi Lucien Favre. Borussia Dortmund mara nyingi imekuwa ikionesha mchezo mzuri kwa dakika chache uwanjani na kisha kupoteana na kusababisha maadui kupenya ngome yao kirahisi. Baada ya pambano hilo alisema.
"Tunapaswa kuendelea kupambana kama hivi. Tumejilinda vizuri, tumekimbia sana. Ilikuwa ni kikosi kimoja cha timu."
FC Kolon ilifanikiwa kwa mara ya kwanza katika muda wa wiki 4 zilizopita kupoteza pointi, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na FC Augsburg ikiwa na kocha wake mpya Markus Gisdol katika mchezo wa pili tangu ashike madaraka. Gisdol alisema baada ya mchezo dhidi ya Augsburg:
"Awali ya yote juhudi tuliyoweka katika mchezo, hasa katika kipindi cha pili, imeturidhisha. Tulipambana , kama nilivyokuwa nikitarajia. Tuliungwa mkono pia na mashabiki wetu. na baada ya hapo ilikuwa tu swali na muda , hadi kupata bao. Tungeweza pia kubadili matokeo ya mchezo huo. Lakini tunaridhika na pointi moja, na kwamba tumeweza kurejea katika mchezo."
Leo jioni mchezo wa 13 wa Bundesliga utakamilika , kwa mchezo kati ya FC Mainz 05 ikiikaribisha Eintracht Frankfurt.