Brexit kupigiwa kura ya tatu Uingereza
29 Machi 2019Wabunge watapata fursa ya tatu leo kuyapigia kura makubaliano ya kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya.
Makubaliano hayo hata hivyo yamekabiliwa na upinzani mkubwa , hata baada ya May kuamua kuiweka rehani kazi yake ili makubaliano hayo yapite, na kuahidi kujiuzulu iwapo wabunge wataidhinisha makubaliano hayo na kuiacha Uingereza ijitoe kutoka Umoja wa Ulaya kama ilivyopangwa mwezi Mei.
Mpambano wa vuta nikuvute nchini humo kuhusu Brexit umesababisha bunge la nchi hiyo kugawanyika na kuunda vikundi hasimu ambavyo dhamira yake na ajenda zinapitia katika misingi ya asili ya chama hicho.
Waziri mkuu Theresa May atajaribu kuwa mchungaji wa makundi hayo yanayovutana na hatimaye kupata wingi ambao kila mara unakosekana ambao utaweza kufanikisha makubaliano yake ya talaka na Umoja wa Ulaya katika jaribio la tatu leo Ijumaa , siku ambayo nchi hiyo ilitamka kwamba itajitoa rasmi katika Umoja huo, siku ya Brexit.
Kiongozi wa baraza la wawakilishi la Uingereza Andrea Leadsom akitangaza kuhusu kura hiyo jana alisema.
"Kama nilivyoliambia bunge wakati nikitoa taarifa yangu mapema leo, hoja iliyowasilishwa na serikali mchana huu imetayarishwa ili kuweza kufuatana na uamuzi wako, Bwana Spika, wakati huo huo ukiakisi nia ya Umoja wa Ulaya kukubali tu kurefusha kifungu 50 hadi tarhe 22 mwezi Mei iwapo makubaliano ya kujitoa yataidhinishwa ifikapo mchana Machi 29."
Tatizo la May
Tatitzo la May linatokana na kushindwa kwake kudhibiti wabunge wa chama chake cha Conservative. Chama hicho ambacho kimsingi kinapendelea wafanyabiashara hakikubaliani kuhusu iwapo Brexit ni mzuri kwa Uingereza, mtazamo ambao May binafsi si mara zote amekubaliana nao, na iwapo Brexit inapaswa kulegezwa ama kuendewa kama ilivyo.
Wapinzani wa dhati ya Umoja wa Ulaya walijaribu kumuondoa madarakani May mwezi Desemba na kisha wakasaidia kushindwa kwa makubaliano aliyofikia katika kura iliyopigwa mwezi Januari na kupata kipigo cha kihistoria kwa kura 432 dhidi ya 202.
Zaidi ya theluthi ya wabunge wa chama hicho wapatao 313 walipiga kura kupinga makubaliano aliyofikia May na Umoja wa Ulaya kila mara yalipofikishwa bungeni.
Idadi ya waasi ilipungua kwa robo wakati mpango wake uliposhindwa tena kwa kura 391 dhidi ya 242 hapo Machi 12. Kiongozi anayeonekana kuwania kiti cha May katika chama Boris Johnson amesema ahadi ya May siku ya Jumatano ya kujiuzulu iwapo makubaliano yake yataidhinishwa ina maana kwamba, "itabidi niunge mkono kitu hicho".