Brexit: Matokeo bado yanakaribiana
21 Juni 2016Hayo ni wakati imesalia siku mbili kabla ya kupigwa kura hiyo ambayo huenda ikaamua hatima ya kisiasa na kiuchumi ya bara la Ulaya. Huku muda ukiyoyoma wa kuwashawishi wapiga kura umati wa maelfu ya watu utakusanyika katika ukumbi wa Wembley Arena kwa ajili ya mdahalo baina ya kambi mbili, utakaomhusisha meya wa zamani wa London Boris Johnson wa kambi ya wanaotaka kuondoka, na mrithi wake Sadiq Khan anayeunga mkono Uingereza kubaki Ulaya.
Matokeo ya karibuni yamegawika kwa nusu, ambapo mawili yanaonyesha kuwa kambi ya wanaotaka kubaki inaongoza lakini utafiti wa tatu unaonyesha kuwa kambi ya wanaotaka kuondoka huenda ikashinda kura hiyo ya Juni 23.
Mtalaamu wa kisiasa Lynton Crosby ameandika katika gazeti la Daily Telegraph kuwa dalili zote zinaonyesha kinyang'anyiro cha kura ya maoni kitaamuliwa katika siku ya mwisho.
Athari katika Umoja wa Ulaya
Kura ya maoni ya Uingereza imefungua uwezekano wa mataifa mengine kudai kura hiyo pia, kitu ambacho labda kinaiweka hatima ya umoja huo wa Ulaya katika hali ya wasiwasi, mradi ambao ulizaliwa kutokana na nia ya kutafuta suluhu ya kudumu baada ya vita vya dunia. Donald Tusk ni Rais wa Umoja wa Ulaya: "hofu kubwa kwangu ni kuwa matokeo hasi yanaweza pia kuzihimiza nchi nyingine zenye wasiwasi katika Umoja wa Ulaya. Yanaweza pia kuwa kitu kama hatua ya kwanza ya mchakato mzima wa kusambaratika. Hilo pia ni kweli kabisa.
Naye kiongozi wa Labour Jeremy Corbyn anayeunga mkono Uingereza kubaki Ulaya, anasema wapioga kura wanaweza kupiga kura ya kuondoka, lakini Umoja wa Ulaya kwa vyovyote vile utastahili kuweka mageuzi.
Tafiti hizo zilifanywa hasa baada ya kifo cha kushtusha cha Jo Cox mbunge wa chama cha Labour aliyekuwa na miaka 41 na mama wa watoto wawili, ambaye alipigiwa rasasi na kuchomwa kisu akiwa njiani kwenda kukutana na umma kaskazini mwa England wiki iliyopita.
Anayedaiwa kumuua, Thomas Mair mwenye umri wa miaka 52, alitoa jina lake kuwa ni “kifo kwa wasaliti, uhuru kwa Uingereza” katika siku yake ya kwanza mahakamani baada ya kushtakiwa kwa mauaji ya mbunge huyo.
Chama kinachopinga Umoja wa Ulaya – UKIP kinatarajiwa kuzindua bango jipya la kampeni, baada ya wakosoaji kulikosoa bango lake la awali – lilionyesha mistari ya wahamiaji wakitembea kote Ulaya na maneno ya “kiwango kibaya” – kuwa ni la kuzusha chuki. Sarafu ya Uingereza Pauni imekuwa katika hali ya kupanda na kushuka wakati kura ya maoni inakaribia na imeanguka tena leo.
Watafiti katika shirika la NatCen wamesisitiza kuwa matokeo ya 50-50 yanaweza kutokea. Magazeti mawili maarufu ya Uingereza, Guardian na Daily Telegraph yameidhinisha pande pinzani za kura hiyo. The Guardian linaunga mkono Uingereza kubakia wakati Daily Telegraph likiwataka wasomaji wake kupuga kura ya kujiondoa Ulaya.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo