Kujitoa Brexit bila makubaliano kutatishia kuvuruga mshikama
30 Mei 2019Katika mahojiano na shirika la utangazaji la Uingereza, BBC, waziri Hammond amesema anatilia shaka iwapo wanasiasa wanaelewa hatari ya kiuchumi iliyopo na mustakabali wa taifa hilo la Uingereza iwapo watatoka katika Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano.
Wabunge kumi na moja wa chama cha Concervative wanawania nafasi hiyo ya waziri mkuu ambapo muwaniaji mmoja Boris Johnson amesema Uingereza itaondoka Umoja wa Ulaya Octoba 31 mwaka huu kwa makubaliano ama hata bila ya makaubaliano.
Hammond ameeleza kwamba hatarajii kinyang´anyiro hicho cha nafasi ya waziri mkuu kuwa mashindano ya nani anaweka ahadi ya fedha nyingi za matumizi au ahadi za kupunguza ushuru na kwamba chama cha Conservative kina hadhi kubwa katika uadilifu wa fedha.
Amewaka wazi kwamba iwapo bungeni kutakuja kura ya kutokuwa na imani na serikali iliyotaka Brexit bila makubaliano basi yeye pia ataunga mkono kura hiyo kwa ajili ya maslahi ya taifa. Huku akisema amekuwa bungeni kwa miaka 22 na hajawahi kupiga kura dhidi ya kinara wa chama cha Conservative kwa hivyo uamuzi wa kuunga mkono kura ya kutokuwa na imani ataufanya sio kwa wepesi ama kwa dhati ya moyo wake.
Uingereza ilijiunga na Umoja wa Ulaya 1973
Alipoulizwa iwapo naye atagombea nafasi hiyo, waziri Hammond hakujibu moja kwa moja bali ameeleza kwamba jukumu lake ni kuhakikisha kuna sauti inayokubaliana na maoni anayoyaamini yeye ya kulimaliza swala la Brexit kwa njia ambayo itazilinda biashara na kazi.
Waziri mkuu mpya atachaguliwa mwishoni mwa mwezi wa saba. Uingereza ilipaswa kutoka Umoja wa Ulaya Machi 29 mwaka huu lakini wanasiasa hawakuwahi kukubaliana juu ya namna gani ya kutoka na kwa wakati gani baada ya taifa hilo kujiunga na umoja huo mwaka 1973.
Brexit bila ya makubaliano inamaanisha kujiondoa kwa mara moja bila ya kuwa na kipindi cha mpito ambapo Gavana wa Benki ya Uingereza Mark Carney anasema kufanya hivyo itafanana na pigo la mafuta walilopata Uingereza miaka ya 1970.
May alikuwa akitahadharisha kwamba Brexit bila ya makubaliano itaathiri kila kitu kuanzia utalii, uagizaji wa dawa muhimu na biashara baina ya Umoja wa Ulaya na mataifa mengine.
(RTRE)