BRICS yakubali wanachama wapya sita
24 Agosti 2023Wanachama hao wapya ni Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Iran, Ethiopia, Argentina na Misri.
Ramaphosa alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa kilele wa kundi hilo mjini Johannesburg.
"Tumekubaliana katika awamu ya kwanza ya upanuzi na nyingine zitafuata. Tumeamua kuwakaribisha Argentina, Misri, Ehtiopia, Iran, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu kuwa wanachama kamili wa BRICS. Uanachama wao utaanza rasmi Januari Mosi mwaka 2024," alisema Ramaphosa.
Miito ya kulipanua kundi hilo, ambalo kwa sasa linaundwa na Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini, ilitawala miongoni mwa ajenda katika mkutano huo wa kilele wa siku tatu na kuibua mgawanyiko miongoni mwa wanachama juu ya kasi na vigezo vya kuwakubali wanachama wapya.
Mkutano huo unahudhuriwa na wakuu wengine 50 wa serikali na mataifa, na unahitimishwa hii leo.