1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga-duru ya kwanza leo

Ramadhan Ali10 Agosti 2007

Msimu wa 2007/8 wa Ligi ya ujerumani ulianza ijumaa kwa kishindo.Na jumamosi hii mabingwa mara kadhaa Bayern munich wanaumana na Hansa Rostock huko Munich.

https://p.dw.com/p/CHbL

Macho ya mashabiki yatakodolewa Allianz Arena, mjini Munich leo ambako Hansa Rostock kutoka mashariki mwa Ujerumani, inadai haifungi safari kwenda Munich kuamkia ,bali kurudi Rostock na pointi 3 mfukoni.

Bayern Munich iliotumia Euro milioni 70 kujiimarisha kwa wachezaji wapya inaingia uwanjani jioni hii kufuta madhambi waliofanya msimu uliopita walipotoka mikono mitupu bila ya taji.

Maadui zao leo ni Hansa Rostock,iliotoka daraja ya pili,lakini iliovinjari kuwaambia wabavaria fedha zenu mlizotumia kununua aykina Luca Toni wa Itali,Riberry wa Ufaransa,Klose wa Ujerumani ni bure.Wamenadi warostock kutoka mashariki mwa Ujerumani kwamba hawaendi leo Munich kupiga picha tu uwanjani au kusema ‘hallo’.Wameapa kutamba na kushambulia.

Werder Bremen,ya tatu katika ngazi ya ligi msimu uliopita inacheza nyumbani mwa Bochum lakini bila ya staid wao Torsten Frings alieumia.Pia Bremen imemuuza Miroslav klose mkuki wao mujarabu kwa Bayern Munich.

Hamburg inatarajiwa pia msimu huu kutamba kwani imemfungisha mkataba Mmisri Mohammed Zidan kutoka Mainz ilioteremshwa daraja ya pili.Inajivunia pia jogoo la Holland Rafael Van der Vaart-nahodha wao.

Bayer Leverkusen iliopigwa kumbo duru ya kwanza ya kombe la shirikisho la dimba la ujerumani mwishoni mwa wiki iliopita wanaania pointi 3 leo kutoka kwa Energie Cottbus-timu ya pili baada ya Rostock kutoka mashariki mwa Ujerumani.

Kocha wa msimu uliopita wa Bayern munich kabla kutimuliwa,Felix Magath anashika msimu huu usukani wa Wolfsburg na mahasimu wao leo jioni ni Armenia Bielefeld.Hertha berlin inaumana na Eintracht Frankfurt.

Kesho duru hii ya kwanza itakamilishwa kwa mapambano 2:Mabingwa wa kombe la shirikisho Nüremberg wana miadi na Karlsruhe iliopanda msimu huu daraja ya kwanza na Borussia Dortmund wanaumana na majirani zao waliopanda pia daraja ya kwanza Duisburg.Duisburg inateremka na mkuki wa Brazil-Ailton aliewahi mara 2 kuwa mtiaji mabao mengi katika bundesliga.

Hata Ligi ya pili ya Ujerumani ni kali mno msimu huu na ni vigumu kubashiri ni timu gani 3 zitapanda mwishoe, daraja ya kwanza:

Timu kama FC Cologne na Borussia Mönch ngladbach zimetumia fedha nyingi kujiimarisha kwa wachezaji wapya kwa lengo la kuhama daraja ya pili kurejea kule zilikozowea kucheza-daraja ya kwanza ya bundesliga.

Cologne ndio inayoongoza kwa mashabiki wake wengi kusheheni viwanjani.Hadi 22.000 na hii haimpi usingizi kocha wake maarufu Christopher Daum.Cologne imefungua msimu jana na St.pauli ya hamburg.Mönchengladbach inataka pia kurudi haraka daraja ya kwanza kama kaiserslauten na hata FC Freiburg.

Katika Premier League-ligi ya Uingereza,kesho jumapili, Arsenal ina miadi na Fulham wakati Chelsea wanakutana na Birmingham City.Manchester United mahasimu wao ni Reading.