1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BUNDESLIGA-HAMBURG YAMTIMUA KOCHA WAKE KURT JARA

23 Oktoba 2003

LEIPZIG NA MICHEZO YA OLIMPIK 2012 VITA VYA KUPAMBANA NA MADHAMBI YA DOPING VYAIMARISHWA NA HSA MAREKANI

https://p.dw.com/p/CHYG

Bundesliga-Ligi ya Ujerumani imerudi uwanjani jioni hii huku klabu zake 2-mabingwa Bayern Munich wanaosimama nafasi ya 5 katika orodha ya Ligi na makamo-bingwa VFB Stuttgart zikijipatia matokeo tofauti katika changamoto za kati ya wiki za champions-league-Kombe la klabu bingwa barani ulaya.
Hamburg imemtimua kati ya wiki hii kocha wake Kurt yara na kumuajiri kocha wa zamani wa Bayer Leverkusen,Klaus Topmmoeller.Hamburg iko nafasi ya 13 ya ngazi ya Ligi na ilipigwa kumbo katika duru ya kwanza tu ya kombe la Ulaya la UEFA.

Kurt jara mwenye umri wa miaka 53 ni Muastria na aliteuliwa kocha wa Hamburg hapo Oktoba mwaka 2001 na kuwaongoza mabingwa hawa wa Bundesliga, 1983 hadi nafasi ya 4 ya ngazi ya Ligi msimu uliopita.msimu huu lakini umeanza vibaya kwa kocha huyu na marekebu yake imekua ikienda mrama na ili isizame kabisa, uongozi wa Hamburg umemtimua na kumteua nahodha mwengine: Topmoeller, mwenye umri wa miaka 52,aliteuliwa kocha wa mwaka mwaka jana baada ya kuiongoza Bayer Leverkuisen kucheza finali ya Kombe la klabu bingwa barani Ulaya na kumaliza pia makamo-bingwa wa Ujerumani ingawa bila kutwaa vikomber vyote viwili.Alitimuliwa na Leverkusen,februari mwaka huu.

Uamuzi wa kumtimua Kurt Jara umekuja kwa msangao kwavile rais wa Hamburg Bernd Hoffmann alisema hapo jumatano tu kwamba Jara angebakia madarakani.tangu kuachana na Leverkusen, kocha mpya Topmoeller, alihusishwa na klabu kadhaa-pamoja na hizo Fulham ya uingereza.Kurt jara ni kocha wa tatu wa Bundesliga kutimuliwa tangu kuanza msimu huu mpya baada ya yule wa B.Mönchengladbach Ewald Lienen na wa hansa Rostock Armin Veh.

Stuttgart inaendelea kutamba tangu katika Bundesliga hata katika Kombe la klabu bingwa barani ulaya:Kati ya wiki hii,Stuttgart ilinyakua ushindi wake wapili baada ya kuizaba Panathinaikos ya Ugiriki katika changamoto za kundi E la champions league. Katika duru ya kwanza Stuttgart ilitandika Manchester United ya uingereza mabao 2:1.Stuttgart kwahivyo, imeparamia kileleni mwa kundi E ikiwa n a pointi 6 kutoka mechi 2.Manchestzer United iliilaza Rangers ya Scotland bao 1:0 na kuondoka pia na pointi 3.

Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich, walimudu sare tu wiki hii na Olympique Lyon ya Ufaransa na katika changamoto kati ya washambulizi wa 2-Giovanne Elber na Roy Makaay, ni Makaay aliewika kwa kutia bao.Elber ameahidi lakini kutia bao katika duru ya pili. Mabingwa watetezi wa Ulaya-AC Milan ya itali, walikiona kilichomtoa kanga manyoya-walizabwa bao 1:0 na >Bruges ya Ubelgiji.

Jiji la Leipzig liliopo mashariki mwa Ujerumani, likifuata nyayo za jiji la berlin, lililoandaa michezo ya olimpik 1936 na Munich,1972, linapigania kuwa mji 3 wa Ujerumani kuandaa michezo hiyo hapo mwaka 2012: Wakati waandazi wa jiji la leipzig wanaieleza michezo hiyo kwa mji wao wa leipzig ni ya kutupa macho usoni,mashetani wa siku zilizopita wamerudi kuupunga mji huu.

Leipzig,ulishinda miji mingine ya Ujerumani katika kinyan'ganyiro cha kuania nafasi hiyo kwa Ujerumani hapo April mwaka huu,lakini mradi wake wa kugombea ulikuja kuchafuliwa mwezi huu pale wawili kati ya wanaoandaa michezo hiyo huko Leipzig,walipobidi kujiuzulu kwa mashtaka ya kuwa wameitumikia Idara ya usalama ya iliokua Ujerumani mashariki-STASI.

Dirk Thaerichen, kiongozi wa kamati inayoongoza kampeni ya jiji hilo kuileta michezo ya olimpik 2012,amekanusha tuhuma kwamba alijiounga na kikosi cha walinzi cha STASI muda mfupi kabla kuporomoka kwa ukuta wa berlin hapo 1989 na kuwa alilenga kujipatia cheo katika chama cha kikoministi kilichotawala Ujerumani Mashariki.

Thaerichen,aliekua chipukizi hapo 1989,alifuata nasaha aliopewa na Bw.Michael Beleites,afisa mwenye dhamana ya kuchunguza dafuitari za STASI katika mkoa wa saxony na hivyo akajiuzulu.Ilidaiwa kuwa jiji la leipzig lina nafasi tu ya kuishinda miji mingine ikiwa litafuta doa la madhambi yaliopita yanayoshikamana na spoti ya iliokua ujerumani mashariki. Katika pigo jengine la juhudi za Liepizig kuandaa Olimpik 2012, Bw.Herald Lochotzke,mkuu mwenye dhamana ya kukuza nafasi za jiji la Rostock kwa mashindano ya olimpik ya mashua ya olimpik,nae alibidi kujiuzulu baada ya kuchomoza tuhuma za kumhusisha pia na Idara ya usalama ya STASI.

Uamuzi wa kuutanguliza mji wa Leipzig badala ya Dusseldorf,Frankfurt,Hamburg au Stuttgart kugombea nafasi hiyo ya maandalio ya Olimpik,ulilengwa kuchangia kufufua uchumi na maendeleo katika sehemu ya mashariki mwa Ujerumani ambayo ingali inapigana kufikia maendeleo sawa na ya wenzao wa Magharibi.Leipzig hata hivyo, inatumai kutumia euro bilioni 2.6 kuandaa michezo ya 2012.leipzig unashindana na miji mikubwa kama London,Paris na New York.Wakaazi wa Leipzig ni laki 5 tu.

VITA VYA KUPAMBANA NA MADHAMBI YA DOPING:

Wakuu wa spoti ulimwenguni wamenadi sasa kweli vita dhidi ya madhambi ya Doping-matumizi ya madawa kuimarisha misuli.Kampeni imeimarishwa kuwafichua na kuwaadhibu wadanganyifu katika michezo.Hii inafuatia wimbi lililopiga wiki hii nchini Marekani kuwa wanariadha kadhaa wanatumia madawa.
Vituo vinavyopiga vita doping kila pembe ya dunia, vimepewa muongozi vipi kugundua mwanariadha alietumia dawa ya THG ambayo imekuwa vigumu kuitambua.

Uchunguzi wa kugundua matumizi ya dawa hiyo ya THG ilitengezwea na Maabara inayoongozwa na prof. Don Catlin katika chuo Kikuu cha California,mjini Los Angeles.Hii ilifuatia kocha asiejitaja dawa hiyo isiojulikana kabla kwa uchunguzi. Shirikisho la riadha ulimwenguni-IAAF limeshatangaza kwamba, litafanya uchunguzi mpya aina zote za mkojo uliochukuliwa wakati wa mashindano ya riadha ya ubingwa wa dunia huko Paris,hapo august kuisaka dawa hii mpya. Wakuu nchini Ufaransa nao wamesema watafanya uchunguzi mpya juu ya kesi 400 . Isitoshe, wakuu wa michezo nchini ujerumani na Ugiriki ambako michezo ijayo ya Olimpik itafanyika,wamesema nao watafanya uchunguzi mpya juu ya mkojo wa wanariadha walioshiriki katika mashindano mwaka huu.

Nae bingwa wa Olimpik wa Uingereza wa masafa ya mita 800 Sebastian Coe, ameungama kwamba baadhi ya majina mashuhuri ya medani ya riadha hayatakuwamo katika michezo ijayo ya Olimpik mjini Athens,mwakani. Halmashauri kuu ya olimpik ulimwenguni-IOC, kati yxa wiki hii ilianza ukaguzi wake wa zana na viwanja vitakavyotumiwa kwa michezo ya mwakani ya Olimpik mjini Athesn,Ugiriki.

Kumekuwapo uvumi kwamba, vyombo muhimu vya usafiri maandalio yake yako nyuma mno.Maafisa wa Halmashauri kuu ya olimpik wakiongozwa na mkaguzi-mkuu Denis Oswald wanatazamiwa kuhimiza hasa kazi ya usafiri wa matram ya majiani na reli kujua maandalio yamefikia wapi.Mji wa Athens, unatarajia zaidi ya watemebzi robo-milioni wakati wa michezo hiyo hapo August,mwakani.