Bundesliga imerudi kwa vishindo
29 Januari 2007Bundesliga-Ligi ya Ujerumani yarudi uwanjani kwa kishindo-kwani mabingwa Bayern Munich wakomewa mabao 3-2 na Borussia Dortmund,katika kombe la klabu bingwa barani Afrika, Young Africans ya Tanzania yapata mchicha –yaoenea ASGM ya Comoro kwa mabao 5-1 mjini Dar-es-salaam na finali ya kombe la Ghuba-Gulf Cup, kesho itakua kati ya Oman na Umoja wa Falme za kiarabu (Emirates).
Bundesliga-Ligi ya Ujerumani imerudi uwanjani kwa vishindo kufuatia likizo ya X-masi na mwaka mpya:Mabingwa Bayern Munich walianza duru ya pili ya msimu kwa pigo kali la mabao 3-2 kutoka viganja vya Borussia Dortmund na ikiwa kesho watashindwa kuilaza Bochum nyumbani ,basi asema kocha wao Felix Magath,taji la msimu huu litakwenda arijojo msimu huu.Bayern Munich hawakuanza uzuri msimu huu na pale Bundesliga ilipokwenda likizoni kwa X-masi, Munich ilijikuta pointi 3 nyuma ya viongozi wa Ligi Werder Bremen.
Kesho Bayern Munich itabidi kucheza bila stadi wao kutoka Holland, Mark van Bommel watakapopambana na Bochum kwani ameumia.Lakini ikishinda kesho, Munich itapunguza mwanya wa pointi 3 kutoka kileleni alao kwa muda wa masaa 24.Bremen siku 1 baadae, ina miadi na Bayer Leverkusen na hapo haitakua kuteremka mlima.Schalke inaonana na Alemania Aachen.
Katika Premier League-Ligi ya Uingereza,Wayne Rooney ameipatia Manchester united ushindi wa mabao 2:1 dhidi ya Portsmouth wakati Arsenal ilimdu suluhu tu bao 1:1 na Bolton Wandereres.Mabingwa Chelsea walishinda mabao 3-0 dhidi ya timu ya daraja ya 3 Nottingham Forest katika kinyan’ganyiro cha kombe la FA.
Huko Spain,mabingwa FC Barcelona walibakia kileleni kufuatia ushindi wao wa mabao 3-1 dhidi ya Celta Vigo.
Na nchini Itali, Inter Milan,haioneshi kuregeza kamba baada ya kuizaba Sampdoria 2-0 na kufungua mwanya wa pointi 11 kileleni.
Nchini Ufaransa, chipukizi Nice ilimudu kuwazima mabingwa Olympique Lyon na kuondoka nao sare bao 1:1.
Rais mpya wa UEFA aliechaguliwa majuzi,mfaransa Michel Platini,alihakikisha jana kwamba anakusudia kutekeleza mpango wake wa kupunguza idadi ya timu zinazowakilisha Uingereza,Spain na Itali, katika kombe la klabu bingwa barani Ulaya.
Platini lakini, ameziofahamu hofu za Uingereza,Spian na Itali kuwa kuanzia 2009 zitabidi kuridhia timu 3 tu za usoni kabisa kutoka Ligi zao kuwakilishwa katika champions League.
Tukigeukia sasa duru ya mwishoni mwa wiki ya kombe la klabu bingwa barani Afrika,mabingwa mara 5 wa kombe hilo Zamalek ya Misri walivuma kwa vishindo kwa kuitimua Vitalo ya Burundi mabao 4:1 mjini Cairo hapo jana .
Katika matokeo mengine, ya Kombe la klabu bingwa barani Afrika, polisi ya Zanzibar ilichapwa mabao 4-0 na Al Hilal ya Sudan, mjini Khartoum.
Young Africans ya Dar-es-salaam ikaionea ASGM ya visiwa vya Comoro kwa mabao 5-1 na inaonywa lakini, isijivunie matokeo hayo na kutamba kwani ASGM kama Polisi ya Zanzibar,bado ni watoto wachanga wanaotambaa katika kombe la klabu bingwa barani Afrika:
Tumalizie Kombe la Ghuba –Gulf Cup:
Kombe hili kesho ama litaelekea Oman au kwa wenyeji Falme za kiarabu –Emirates.Katika finali ya kombe la 18 la nchi za Ghuba lililoanzishwa 1970, si Oman wala Emirates iliowahi kulinyanyua kombe hili.Oman iliitoa Bahrein kwa bao 1:0 wakati wenyeji Emirates iliipiga kumbo Saudi Arabia-mabingwa mara tatu wa kombe hilo.
Katika Kombe la dunia la mpira wa mkono-handball-Ujerumani itapaswa leo kuwika mbele ya mabingwa watetezi Spain ikiwa inataka kweli kukata tiketi yake hadi nusu-finali.Ujerumani iliitoa Iceland jana kwa mabao 33-28 katika finali ya kundi lao .