1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga katika mawindo makali

Aboubakary Jumaa Liongo19 Julai 2010

Hapa Ujerumani. Baada ya kumalizika kwa fainali za kombe la dunia ambapo timu yake ya taifa iliyoundwa na vijana ilikamata nafasi ya tatu, sasa pilika pilika ni katika mawindo kabla ya kuanza Bundesliga

https://p.dw.com/p/OPPW
Kiungo wa Stuttgart Sami Khedira,Picha: AP

Vilabu vimekuwa katika mikakati ya kuimarisha vikosi vyao, kwa kuzuia wasiondoke ama kusajili wapya.

Wachezaji wa timu ya Ujerumani kutokana na kabumbu lao wamekuwa wakiwindwa hivi sasa na vilabu mbalimbali barani Ulaya:

Miongoni mwao ni Sami Khedira kiungo wa Stuttgart aliyeripotiwa kujiunga na Real Madrid ya Uhispania. Kocha wa Real Jose Morinho alinukuliwa akisema kuwa anammezea sana mate kiungo huyo.

Hata hivyo  leo hii Khedira amenukuliwa na jarida la spoti hapa Ujerumani liitwalo Kicker akikanusha kujiunga na Real, lakini hata hivyo amesema yu radhi na furaha kujadiliana na viongozi wa Sttutgart juu ya mpango wa kuihama klabu hiyo.

Mapema vyombo vya habari vya Uhispania viliarifu kuwa Khedira mwenye umri wa miaka 23 ameingia mkataba wa kuichezea Real Madrid hadi mwaka 2015.

Morinho pia alitangaza kuwa anataka kumsajili chipukizi mwengine wa Ujerumani anayechezea Werder Bremen, Mesut Oezil.

Kwa upande mwengine, mchezaji wa klabu ya Hoffenheim mghana Isaac Vorsah atachelewa kujiunga na mawindo ya klabu yake kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi kutokana na kufiwa na kaka yake huko Ghana.

Vorsah alikuwepo katika kikosi cha Ghana kilichofika hatua ya robofainali ya kombe la dunia huko Afrika Kusini. Pia mchezaji mwenzake wa Ghana Prince Tagoe wanaochezea pamoja Hoffenheim atachelewa katika mawindo hayo kwani atakuwa pamoja na rafiki yake kwenye msiba huo.

Kwa ujumla lakini, ligi ya Bundesliga msimu huu inaonekana itakuwa kali zaidi na kiwango kilichooneshwa na timu ya Ujerumani nchini Afrika Kusini, kimethibitisha kurejea kwa Bundesliga katika kilele cha ligi ngumu kabisa duniani.

Huko nchini Uingereza, timu ya Liverpool, katika kuhakikisha inakuwa tishio msimu ujayo, leo imemsajili mshambuliaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo na Chelsea, Joe Cole, kwa mkataba wa miaka minne.

Joe Cole pamoja na nahodha wa Ujerumani Michael Ballack walifunguliwa mlango na Chelsea na kuambiwa ondokeni. Ballack amerejea katika Bundesliga kwenye klabu yake ya zamani Bayer Leverkusen

Mwandishi:Aboubakary Liongo

Mhariri: Josephat Charo