Bundesliga mapumzikoni, RB Leipzig mabingwa duru ya kwanza
23 Desemba 2019RB Leipzig imekaa kileleni mwa msimamo wa ligi ya Ujerumani , Bundesliga , wakati ligi hiyo ikienda mapumziko ya majira ya baridi na sikukuu ya Krismas, ikiiondoa Borussia Moenchengladbach iliyokuwa katika nafasi hiyo kwa muda mrefu wa sehemu hii ya kwanza ya michezo 17 ya ligi.
RB Leipzig ina pointi 37, ikiipita Gladbach kwa pointi 2, wakati mabingwa watetezi Bayern Munich wako nafasi ya tatu wakiwa na pointi 33. makamu bingwa Borussia Dortmund imeshindwa kusogea katika nafasi ya tatu baada ya kupata kipigo bila kutegemea cha mabao 2-1 dhidi ya TSG Hoffenheim siku ya Ijumaa. Dortmund iko nafasi ya 4 ikiwa na pointi 30. Kocha wa RB Leipzig Julian Nagelsmann ameimwagia sifa timu yake kwa kuwa mabingwa wa majira ya mapukutiko.
"Tumo katika mashindano yote, tumepata matokeo mazuri katika bundesliga. Nafurahia kwa hilo, ambapo tunapata muda kidogo wa kupumua. Nafurahi lakini pia , hapo Januari 6 kila kitu kinaanza upya kwa mazowezi na iwapo tunaweza kujiongeza zaidi kidogo. Sisi pia tunapaswa kufanya hivyo. Tuna uwezo wa kutosha katika kikosi chetu, na hii ni safi kabisa. Na wakati mzunguko wa pili utakwenda vizuri kama duru hii , tunaweza bila shaka kufanya vizuri."
Schalke 04 imemaliza mzunguko huu kwa kukaa karibu na hasimu wake mkubwa Borussia Dortmund , timu hizo hizo zikiwa na pointi 30 katika nafasi ya 4 na 5. Timu iliyopata mafanikio makubwa katika michezo ya mwisho ya duru hii ni FC Koln ambayo chini ya kocha wake mpya Markus Gisdol imefanikiwa kupata pointi 9 katika michezo mitatu ya mwisho. Huyu hapa kocha wa FC Koln Markus Gisdol.
"Iwapo tungefikiri , kwamba tungeweza kupata pointi tisa katika wiki hii ya michezo ya kila baada ya siku tatu, dhidi ya timu ambazo tumecheza nazo, bila shaka tungesema, kwamba tumeonesha ujasiri mkubwa. Lakini kwa kweli tunafuraha nyingi. Sasa tunaweza kusherehekea krismas. Lakini bila shaka hapo mbeleni hatuwezi kushinda michezo yote. Hakuna sababu kwa mtu hapa Koln kuanza kuota. lakini kutokana na jinsi tulivyocheza, tunaweza kujenga juu ya msingi huo."
FC Koln imechupa kutoka nafasi ya mwisho ya ligi hadi nafasi ya 15, ikiwa na pointi 17, ikifuatiwa na Fortuna Dusseldorf yenye pointi 15, Werder Bremen yenye pointi 14 na ya mwisho inayoshikilia mkia ni SC Paderborn iliyosalia na pointi 12 licha ya kupata ushindi w mabao 2-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt katika mchezo wa mwisho wa duru ya kwanza.
Wakati huo huo mchezaji wa Bayern Munich Javi Martinez anakabiliwa na karibu wiki 6 nje ya uwanja baada ya kupata maumivu ya misuli katika mchezo wa Jumamosi ambapo timu hiyo ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya VFL Wolfsburg, amesema kocha wa muda wa timu hiyo Hansi Flick.