Bundesliga: Wolfsburg yaibuka
12 Novemba 2012Katika Bundesliga, pambano ambalo limezikutanisha timu mbili zinazoshiriki katika michuano ya ligi ya Ulaya Stuttgart na Hannover , limemalizika kwa ushindi mnono wa kikosi cha kocha Mirko Slomka Hannover 96 wa mabao 4-2.
Kocha wa Mirko Slomka anayepigiwa upatu kuiongoza Bayern Munich mara msimu huu utakapomalizika ama kurejea tena katika timu yake ya zamani ya Schalke 04 alionyesha furaha yake kwa ushindi huo, lakini pia amesema alikosa usingizi kabla ya mchezo huo na Stuttgart.
"Tumefurahi sana kwa ushindi huu dhidi ya Stuttgart ngumu, kama ilivyoonekana wiki iliyopita na tuliingia uwanjani kwa kuiheshimu sana timu hii. Ndio sababu basi tunafuraha kubwa , kwamba tumeweza kupata mafanikio".
Borussia Moenchengladbach ilisherehekea ushindi wake wa 600 tangu Bundesliga ianze baada ya kuizamisha Greuther Fürth iliyopanda daraja msimu huu kwa mabao 4-2.
Leverkusen hoi
Baada ya michezo kumi bila kushindwa Bayer Leverkusen ilisalim amri mbele ya VFL Wolfsburg jana Jumapili(11.11.2012) kwa kipigo cha mabao 3-1. VFL Wolfsburg iliyoachana na kocha wake aliyeitawaza mabingwa Felix Magath , na kuongozwa na kocha wa mpito Lorenz-Günther Köstner ilikuwa mwiba kwa Leverkusen jana. Leverkusen ilionyesha udhaifu mkubwa katika ulinzi.
Msimamo wa ligi ya Bundesliga haujabadilika, ambapo FC Bayern Munich ikiongoza ikiwa na points 30 ikifuatiwa na Schalke 04 ambayo ina points 23, Einchracht Frankfurt iko katika nafasi ya tatu ikiwa na points 20, na inafuatiwa na mabingwa watetezi Borussia Dortmund ambayo ina points 19 hadi sasa.
Di Matteo anahofu
Na huko katika Premier League nchini Uingereza , kocha wa Chelsea FC Roberto Di Matteo anahofu ya kutokea mabaya zaidi baada ya John Terry kupata maumivu katika goti katika mchezo wa jana jioni kati ya timu hiyo na Liverpool ambapo matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.
Nahodha huyo wa Chelsea ambaye alikuwa anarejea dimbani baada ya kupigwa marufuku kushiriki katika michezo minne ya ligi atafanyiwa uchunguzi leo(12.11.2012) kuangalia hali ya goti lake. Aligongana na mshambuliaji wa Liverpool Luis Suarez na kupata maumivu hayo.
Na katika La Liga, nchini Hispania Atletico Madrid imefanikiwa kukaa karibu ya viongozi wa ligi hiyo Barcelona kwa kutengana kwa points tatu tu wakati jana Jumapili walipofanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya majirani zao Getafe.
Kabla ya hapo Barcelona ilifanikiwa kuiangusha Mallorca kwa mabao 4-2.
Wakati huo huo mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo atafanyiwa uchunguzi leo baada ya kupata jeraha juu ya jicho lake la kushoto wakati wa mchezo kati ya Real na Levante ambapo mabingwa hao watetezi walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Viongozi wa ligi ya Ufaransa Paris St German wamemlalamikia mwamuzi baada ya kutolewa nje mlinzi wao Mamadou Sakho kwa kadi nyekundu na kuambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Montpellier jana Jumapili(11.11.2012).
Nae mchezaji nyota wa Chelsea Frank Lampard huenda akajiunga na wachezaji wenzake wa zamani katika kikosi cha Chelsea Didier Drogba na Nicolas Anelka kwa kuhamia katika ligi ya China , baada ya klabu ya Guizhou Renhe kudhibitisha leo kuwa inafanya mazungumzo nae.
Gor Mahia yajuta
Katika bara la Afrika : Huko nchini Kenya Tusker imefanikiwa kurejesha taji lake la ubingwa wa ligi ya nchi hiyo mwishoni mwa juma wakati ligi ya nchi hiyo ilipofikia tamati , kwa msisimko wa aina yake ambao ulihusisha timu tatu.
Tusker imeshinda ubingwa huo ikiwaacha nyuma vigogo wa soka wa nchi hiyo Gor Mahia ambayo ilipigiwa upatu kulinyakua kombe hilo kwa mara ya kwanza baada ya kusubiri kwa muda wa miaka 17, halikadhalika na AFC Leopards.
Kushindwa Gor Mahia kulibeba kombe hilo kulisababisha mashabiki kupandwa na hasira na kufanya ghasia na kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Kenya watu wawili walifariki kutokana na ghasia hizo.
Simba wasi wasi
Na huko Tanzania, ligi ya Premier League , Tanzania bara imemaliza duru yake ya mwanzo. Simba ambayo ni mabingwa watetezi imefanya vibaya katika michezo yake ya mwisho kuelekea mwisho wa duru hii ya kwanza na hali kama hiyo kwa vigogo wa ligi ya Tanzania huashiria mgogoro.
Timu hiyo imebamizwa na Toto Africa ya Mwanza kwa bao 1-0 mwishoni mwa juma na pia iliangukia pua ilipopata kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Turiani Morogoro.
Wakati huo huo michuano ya kuwania ubingwa wa mataifa ya Afrika mashariki na kati itaanza rasmi tarehe 24 Novemba katika uwanja wa Namboole mjini Kampala na makundi yalipangwa jana usiku.
Kundi A lina timu za mabingwa watetezi Uganda, Kenya , Sudan ya kusini na Ethiopia. Kundi B lina timu za Sudan, Tanzania, Burundi na Somalia, wakati kundi C litajumuisha timu za Rwanda , Malawi, Zanzibar na Eritrea.
Katika maandalizi ya michuano hiyo, timu za Taifa Stars ya Tanzania na Kenya Harambee Stars zinakutana katika uwanja wa CCM Kirumba siku ya Jumatano kwa mchezo wa kirafiki.
Timu zajiandaa
Timu zinazotarajiwa kunyakua ubingwa wa mataifa ya Afrika kama Cote D'Ivoire ni miongoni mwa timu 14 zilizofuzu kucheza katika fainali za kombe hilo mwakani ambazo zimeanza matayarisho kwa ajili ya michuano hiyo kwa kucheza michezo mbali mbali ya kirafiki katika bara la Afrika, Ulaya na Amerika ya kaskazini.
Ghana na Cape Verde zinaanza majaribio kesho mjini Lisbon zikifuatiwa na michezo 15 siku ya Jumatano mjini Miami, ambapo Nigeria inapambana na Venezuela, na mjini Johannesburg ambapo Bafana bafana inakwaana na mabingwa watetezi wa kombe la Afrika Zambia.
Cote D'Ivoire inapambana na Austria.
Kwa taarifa hizo mpenzi msikilizaji ndio sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea habari hizi za michezo jioni ya leo. Jina langu ni Sekione Kitojo, hadi mara nyingine kwaherini.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae
Mhariri: Josephat Charo