Bundesliga yaingia kipindi cha mapumziko
21 Desemba 2012Lakini kwa mujibu wa nyota wa Bayern Bastian Schweinsteiger, mabingwa wa Ujerumani Borussia Dortmund watabaki kuwa moto wa kuotea mbali katika kipindi cha pili na cha mwisho cha msimu mwaka wa 2013, licha ya kuwa wanajikokota katika kinyang'anyiro cha taji la Bundesliga.
Bayern wamemaliza kipindi cha kwanza cha msimu na uongozi wa tofauti ya pointi tisa wakati Dortmund wakiwa nyuma na tofauti ya pointi 12 katika nafasi ya tatu, wakati wakiingia katika kipindi hiki cha mapumziko cha wiki nne ya msimu wa theluji.
Mabingwa watetezi wa kombe la DFB Pokal Dortmund watatua katika uwanja wa Allianz Arena katika mchuano wa Februari wa robo fainali, na wakati timu hizo zote mbili zikiwa zimefuzu katika awamu ya muondowano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Champions League, Schweinsteiger anasisitiza kwamba Dortmund ndiyo timu itakayosababisha ushindani mkubwa.
Aliyekuwa mkufunzi wa Real Madrid Bernd Schuster anatarajiwa kuchukua usukani kama kocha wa klabu inayokumbwa na masaibu ya Bundesliga VfL Wolfsburg baada ya kaimu kocha Lorenz-Guenther Koestner kumaliza muhula wake Alhamisi. Koestner tayari ameiaga timu hiyo siku moja baada ya Wolfsburg kufika robo fainali ya kombe la shirikisho Ujerumani kwa kuizaba Bayer Leverkusen magoli mawili kwa moja. Alikuwa uongozini tangu mwezi Oktoba baada ya kutimuliwa Felix Magath.
Magazeti ya kila siku ya Kicker Sports na Bild yamesema Schuster atasaini mkataba wa hadi mwaka wa 2015. Mabingwa hao wa mwaka wa 2009, Wolfsburg wako katika nafasi moja tu mbele ya eneo la kushushwa daraja katika nafasi ya 15. Schuster hajawahi kuifunza klabu ya Bundesliga hapo kabla, lakini aliiongoza Cologne katika divisheni ya pili mwaka wa 1998 – 1999. Amezifunza timu nchini Ukraine, Uhispania, Uturuki na kuongoza Real katika kunyakua taji la Ligi ya Uhispania.
Katika habari za soka ya Afrika ni kwamba mchezaji wa Cote d'Ivoire, Yaya Toure, ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika, ya shirikisho la CAF, kwa kuwabwaga mwenzake Didier Drogba na Alexandre Song wa Cameroon.
Toure mwenye umri wa miaka 29 amenyakua tuzo hiyo kwa mwaka wa pili mfululizo, na kumaliza msimu ambao aliisaidia klabu yake ya Uingereza, Manchester City, kutwaa taji la Ligi kwa mara ya kwanza katika miaka 44.
Kwingineko, Gabon imeadhibiwa kwa kunyimwa ushindi wa magoli matatu kwa sifuri kwa kumshirikisha mchezaji asiyefaa katika mchuano wa kufuzu kwa kombe la dunia ugenini dhidi ya Niger mjini Niamey mnamo Juni tatu mwaka huu ambao uliishia sare ya bila kufungana.
Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA imeyabatilisha matokeo hayo baada ya kuamua kwamba beki wa Gabonn, Charly Moussono, hakustahili kucheza kwa sababu awali alikuwa ameichezea Cameroon. Takwimu za FIFA zinaonyesha kwamba Moussono aliichezea Cameroon katika kombe la dunia la kandanda ya ufukweni nchini Brazil mwaka wa 2006.
Uamuzi huo una maana kwamba Gabon wameteremka hadi nafasi ya tatu katika kundi E la kufuzu katika mechi za kombe la mataifa ya Afrika na pointi tatu kutokana na mechi mbili, sawa na Niger na moja nyuma ya viongozi wapya Congo. Burkina Faso ambayo ina pointi moja ni timu nyingine katika kundi hilo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri:Josephat Charo