1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga yaingia mapumziko ya kipupwe

Admin.WagnerD21 Desemba 2015

Hapa Ujerumani katika ligi ya Bundesliga, nusu msimu umemalizika mwishoni mwa juma na ligi hiyo itarejea tena viwanjani mwishoni mwa Januari.

https://p.dw.com/p/1HRIB
DFB Pokal Bayern München Darmstadt 98 SPERRFRIST
Picha: Getty Images/A.Hassenstein

Katika mchezo wa 17 wa ligi hiyo Bayern Munich bado inaendelea kutunisha misuli , baada ya kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Hannover 96 timu ambayo imeendelea kufanya vibaya katika ligi hiyo ikiwa katika nafasi ya 17 katika ligi yenye timu 18.

mlinda mlango wa Bayern Manuel Neuer amejitetea kuhusiana na mshindi huo mwembamba kwamba hauhusiani na kocha nyota Pep Guardiola kuiacha mkono timu hiyo lakini ni miguu imekuwa mizito baada ya heka heka za mwaka mzima huu. "Katika kipindi cha kwanza tulipoteza nafasi moja ama mbili, na hii haikutufurahisha. Na kisha nadhani tulipunguza kasi katika kipindi cha pili. Lakini tunafurahi kuondoka na ushindi wa bao 1-0.

Bundesliga 17. Spieltag FC Köln - Borussia Dortmund
Dortmund inashikilia nafasi ya pili kwenye BundesligaPicha: Getty Images/Bongarts/D.Grombkowski

Timu iliyoko katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi hiyo Borussia Dortmund ilikwaa kisiki mjini Kolon , pale ilipokubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya 1 FC Koln na kocha Thomas Tuchel hakukosa la kusema kuhusu kipigo hicho. "Leo inauma, kama ilivyo kwa kipigo chochote inauma. Kuna sababu yake na inatupasa kuifanyia kazi. Tulipaswa kurejea kabisa katika eneo letu katika kipindi cha kwanza, lakini hatukufanya hivyo. Kwa sasa tuna muda kiasi wa kujipumzisha na kupata tena nguvu.

Timu ambayo imeendelea kufufuka katika kipindi cha mwisho kabla ya mapumziko ni Augsburg ambayo imepata ushindi mfululizo mara tatu na siku ya Jumamosi ilifanikiwa kukamilisha mapumziko kabla ya Chrismass kwa ushindi mnono wa bao 1-0 dhidi ya Hamburg SV. Kocha wa Augsburg markus Weinzierl amezungumzia kuhusu mafanikio hayo. "Hatukuwa wenye kufanya mambo kwa makini, ama sivyo tungeshinda kwa idadi kubwa ya mabao. Lakini tulikuwa watulivu sana na hatari sana leo. Sifa nyingi nazitoa kwa timu yangu mwishoni mwa juma la michezo mfululizo kwa kucheza kama ilivyocheza na kupata mafanikio makubwa hapa Hamburg.

Timu iliyoshangaza ya Hertha Berlin imeendelea kujiimarisha katika nafasi ya tatu kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mainz 05 jana Jumapili, ukiwa ni ushindi wao wa tano katika michezo sita.

Wakati huo huo kocha wa Hannover 96 Michael Frontzeck amejiuzulu wadhifa wake, klabu hiyo imetangaza hii leo.

Frontzeck mwenye umri wa miaka 51 ambaye alichukua kazi hiyo ya kuifunza Hannover mwishoni mwa msimu uliopita, amesema anahisi haaminiki tena na waajiri wake.

Nae mshambuliaji wa Barcelona Luis Suarez ameonya kwamba vigogo hivyo kutoka Uhispania vitaendelea kuwa na kiu ya mataji mengi zaidi baada ya kunyakua taji la ubingwa wa dunia kwa vilabu jana.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman