1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga yaingia mapumzikoni

23 Desemba 2013

Ligi kuu mbalimbali za soka barani Ulaya zimeingia katika kipindi kifupi cha mapumziko ya majira ya theluji, ambapo hapa Ujerumani Bayern Munich, wanaukamilisha mwaka wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi.

https://p.dw.com/p/1AfFS
FIFA Klub Weltmeisterschaft Bayern München vs Raja Casablanca
Picha: Reuters

Bayern walinyakua taji lao la tano katika mwaka wa 2013 baada ya kuwazaba Raja Casablanca wa Morocco magoli mawili kwa sifuri katika fainali ya Kombe la Dunia la Vilabu mjini Marrakech mwishoni mwa wiki. Hii ina maana kuwa kabati lao lina Kombe la Mabingwa Ulaya, Taji la Bundesliga, Kombe la Shirikisho DFB, European Super Cup na Kombe la Dunia la Vilabu.

Na wakati vigogo hao walipokuwa wakitafuta taji la tano nchini Morocco, mahasimu wao katika Bundesliga Borussia Dortmund na Bayer Leverkusen walizidiwa nguvu na kushindwa katika mechi zao. Na hivyo kuwapa Bayern uongozi wa pengo la pointi 12 kileleni. Bayern wameweka rekodi ya magoli 41 katika mechi za Bundesliga, bila kushindwa mchuano wowote, na msimu huu wameshinda 14 na kutoka sare mechi mbili kati ya 16 walizocheza.

Wakati huo huo, Borussia Dortmund ambao wamekuwa mahasimu wao wakuu, wameyumba katika siku za karibuni, wakati kocha Jurgen Klopp akikabiliwa na wakati mgumu wa kuyaweka mambo sawa kutokana na kukosekana wachezaji wake nyota ambao wako mkekani wakiuguza majeraha.

Dortmund walishindwa nyumbani na Hetha Berlin magoli mawili kwa moja na wamepoteza michuano yao mitatu ya nyumbani kwa mara ya kwanza tangu Aprili 2008 na wamepata point nne tu kutokana na mechi zao sita za mwisho. Bayer Leverkusen waliumaliza mwaka kwa kichapo cha goli moja kwa sifuri na Eintracht Frankfurt na kingine cha moja kwa sifuri lakini mara hii mikononi mwa Werder Bremen.

Kocha wa Hannover Mirko Slomka na mwenzake wa Schalke Jens Keller wataendelea kuhudumu
Kocha wa Hannover Mirko Slomka na mwenzake wa Schalke Jens Keller wataendelea kuhudumuPicha: Bongarts/Getty Images

Dortmund na Leverkusen, sasa watalazimika kuwa chonjo dhidi ya Borussia Moenchengladbach na Wolfsburg ambao wanaonekana kukimbia kwa kasi. Hertha Berlin sasa wako katika nafasi ya sita point sawa na Schalke ambao kocha wao Jens Keller amekuwa akikabiliwa na mbinyo.

Lakini sasa hayo yote yamesuluhishwa baada ya klabu hiyo kuthibitisha kuwa Jens Keller ataendelea kuhudumu kama kocha wake wakati duru ya mwisho ya msimu ikianza 2014. Taarifa kutoka kwa klabu hiyo imesema kuwa mambo yote yamejadiliwa na kueleweka kuhusu kile kitakachorekebishwa.

Kocha wa Hanover Mirko Slomka pia amekuwa chini ya shinikizo baada ya kichapo cha mabao mawili kwa moja na Freiburg, lakini mkurugenzi wa klabu Martin Kind amesema kocha huyo ataendelea kuhudumu katika klabu hiyo.

Nuremberg iliweka rekodi mpya ya kutoshinda mchuano hata mmoja katika duru ya kwanza ya msimu, baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Schalke 04. na sasa kocha wake Mholanzi Gertjan Verbeek ameahidi kuwa hatanyoa ndevu hadi watakapopata ushindi wao wa kwanza wa msimu, hata kama ataonekana kuwa kama Satan Claus au Father Christmas. Nuremberg sasa wametoka sare mechi 11 kufikia sasa msimu huu, na wanashikilia mkia pointi 11 sawa na Eintracht Braunschweig, ambao walipata ushindi wao wa tatu msimu huu wagoli moja kwa sifuri dhidi ya Hoffenheim.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu