Bundesliga yaingia wiki ya pili
19 Agosti 2013Hertha BSC Berlin baada ya kuanza vizuri msimu huu wa ligi kwa kuikandika Eintracht Frankfurk kwa mabao 6-1 baada ya mchezo wao wa kwanza katika bundesliga baada ya kufanikiwa kurejea tena katika daraja hilo, imebidi kukubali hali halisi. Hertha iliridhika na sare ya mabao 2-2 dhidi ya FC Nürnberg jana Jumapili.
Makamu bingwa wa Bundesliga Borussia Dortmund ilitoka jasho katika ushindi wake wa mabao 2-1 nyumbani jana dhidi ya timu iliyopanda daraja msimu huu ya Eintracht Braunschweig. Borussia ilihitaji bao la dakika ya 68 la mchezaji wa akiba Jonas Hofmann na penalti iliyowekwa wavuni na Marco Reus kuweza kuuvunja ukuta mgumu wa Braunschweig jana Jumapili katika mchezo wa kukamilisha wiki ya pili tangu kuanza kwa Bundesliga.
Chipukizi Jonas Hofmann wa Dortmund amejisikia furaha kufanikisha ushindi wa timu yake.
"Kabla ya kocha kuamua niingie uwanjani pia alisema natakiwa kucheza kwa kufurahia mchezo, na kuonyesha uwezo wangu kwa asilimia 100 kama ilivyo katika mazowezi , na nafikiri , hilo nimelitimiza leo".
Kocha wa Braunschweig Torsten Lieberknacht hata hivyo amesema kuwa ni vigumu kuidhibiti Borussia iwapo unapunguza kasi katika mchezo.
"Leo imeonekana wazi kuwa Dortmund kwa mara nyingine tena ina kasi kubwa wakati wa kushambulia na wameweza kirahisi kuidhibiti hali, kwamba wakati nguvu zilianza kutuishia wao walikuwa bado wana uwezo".
Kwa upande wa Hertha BSC Berlin ambao walilazimika kuachia usukani wa ligi baada ya ushindi wa kishondi wiki iliyopita , kocha Jos Luhukay amesema ni mwanzo mzuri kwa timu yake.
"Hatujishughulishi kabisa na kuongoza ligi, nisema hivyo wiki iliyopita. hatuwezi kupambana kukaa juu ya msimamo wa ligi, tunalazimika kujitahadhari kwa kila hali".
Mabingwa watetezi Bayern Munich ilibidi kupata ushindi mgumu dhidi ya Eintracht Frankfurt , ambapo mabingwa hao wa Bundesliga na Champions League walitosheka na ushindi wa bao 1-0 siku ya Jumamosi.
Baada ya michezo miwili Borussia Dortmund inashikilia usukani kwa kuwa na points 6 , ikiwa pia na mabao 6 na ikifuatiwa na mabingwa watetezi Bayern Munich pia ikiwa na points 6.
Jose Mourinho amelakiwa kwa shangwe kubwa jana(18.08.2013) uwanjani Stanford Bridge mjini London kabla ya kikosi chake cha Chelsea kuidhibiti Hull City Tigers kwa mabao 2-0 katika ligi ya Uingereza Premier League.
ManU kidedea
Kocha wa mabingwa Manchester United David Moyes alionja ushindi akiwa na timu yake mpya wa mabao 4-1 dhidi ya Swansea City , lakini Arsenal ilipata kipigo cha kushtukiza cha mabao 3-1 dhidi ya Aston Villa nyumbani na kusababisha wapenzi wa timu hiyo kuongeza mbinyo kwa kocha wa muda mrefu wa timu hiyo Arsene Wenger kwa kuiambia bodi ya klabu hiyo kuwa haitakuwa sahihi kumpa Mfaransa huyo mkataba mpya.
Mkataba wa wenger unamalizika mwishoni mwa msimu huu lakini baada ya kushindwa kupata taji katika miaka nane iliyopita , kocha huyo mwenye umri wa miaka 63 kiti chake kinalega lega kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya miaka 17 ya kuiongoza timu hiyo ya kaskazini mwa jiji la London.
Chelsea kuanza enzi mpya
Jose Mourinho anaamini kuwa Chelsea iko tayari kuingia katika enzi mpya baada ya kutokea mgawanyiko katika klabu hiyo na kuigawa msimu uliopita. katika siku ambayo mmiliki wa klabu hiyo Roman Abramovich ameadhimisha mwaka wa 10 tangu kujihusisha na klabu hiyo ya Stamford Bridge , Mourinho amesema na hapa namunukuu : " Unaweza kuona kile Chelsea ilichofanya katika miaka 10 iliyopita, kwa hiyo nafikiri ni vizuri kuangalia kuhusu hilo badala ya kuangalia sehemu zilizokwenda kombo katika historia ya klabu hiyo.
Manchester City iliyoshika nafasi ya pili katika ligi ya Uingereza msimu uliopita inakwaana na Newcastle leo Jumatatu.
Nchini Uhispania kocha mpya wa mabingwa wa La Liga Barcelona Gerardo Martino ameanza kazi yake kwa kishindo baada ya kikosi hicho kuirarua timu dhaifu ya Levante kwa mabao 7-0 uwanjani Nou Camp katika mchezo wao wa mwanzo wa La Liga jana Jumapili.
Kwa upande mwingine kocha mwingine mpya katika La Liga Carlo Anceloti alikuwa na wakati mgumu baada ya ushindi wa mabao 2-1 wa Real Madrid dhidi ya Real Betis.
Wakati huo huo Atletico Madrid inapambana siku ya Jumatano na FC Barcelona katika mchezo wa kwanza katika kombe la Super Cup nchini Uhispania.
Nchini Italia Carlos Tevez akiichezea Juventus Turin kwa mara ya kwanza katika ligi ya Italia Serie A alipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Lazio Rome.
Nayo Paris St. Germain ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Ajaccio katika ligi ya ufaransa League 1 na makamu bingwa wa ligi hiyo Olympique Marseille ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Evian Thonon Gaillard, ikiwa ni moja kati ya timu zilizofanikiwa kupata ushindi katika michezo yote ya mwanzoni mwa ligi ikiwa ni pamoja na Monaco, Olympique Lyon na St. Etienne.
Champions League
Wakati huo huo Schalke 04 na Arsenal London zitajaribu kuweka kando mwanzo mbaya katika ligi za nyumbani msimu huu wakati zikiwania kufikia katika awamu ya makundi ya Champions League. Schalke 04 inaikaribisha PAOK Thessaloniki siku ya Jumatano baada ya kipigo cha mabo 4-0 dhidi ya wolfsburg katika Bundesliga siku ya Jumamosi , kipigo kilichofuatia sare ya mabo 3-3 dhidi ya Hamburg SV wiki moja iliyopita na mshambuliaji Klaas-Jan Huntelaar akiwa nje akiwa ni majeruhi.
Mchezo huo utaileta timu hiyo uso kwa uso na kocha wake wa zamani Huub Stevens ambaye anaifunza PAOK Ssaloniki, na alifutwa kazi na klabu hiyo ya Bundesliga Desemba mwaka jana.
Arsenal London ambayo inawania kufika katika awamu ya makundi kwa mara ya 16 mfululizo , inapimana nguvu na Fenerbahce timu ambayo inapambana kubakia katika mashindano hayo ya Ulaya kufuatia kufungiwa na shirikisho la soka la Ulaya UEFA.
Hatua ya kufungiwa Fenerbahce imesitishwa kwa muda kutokana na klabu hiyo ya Uturuki kukata rufaa kwa mahakama ya upatanishi ya michezo mjini Lausanne Uswisi, ambapo uamuzi unatarajiwa kabla ya kupangwa kwa michezo ya makundi wiki ijayo. Michezo mingine siku ya Jumatano ni kati ya Dinamo Zagreb dhidi ya Austria Vienna , Ludogorets wa Bulgaria inapambana na Basel ya Uswisi na Steaua bucharest na Bulgaria ina kibarua na Legia Warsaw ya Poland.
Kesho lakini AC Milan inamiadi na PSV Eindhoven, Real Sociedad inasafiri kwenda nchini Ufaransa ambapo itapambana na Olympique Lyon , Shakhtar Donetsk ya Ukraine inatiana kifuani na Celtic Glasgow.
Riadha.
Michezo ya riadha ya ubingwa wa dunia imemalizika jana Jumapili mjini Moscow na michezo hiyo imeonesha kuwa kumuangusha Usain Bolt kutoka kiti chake cha ufalme kunaweza kuchukua muda mrefu kidogo wakati bado nyota huyo wa mbio fupi anawapa changamoto kubwa washindani wenzake.
Wakati bado kasi yake ni kubwa mno , wengine wanafanyakazi ya ziada kupambana na mtu huyu mwenye kasi kubwa duniani akirejea nyumbani kutoka katika mashindano hayo ya ubingwa wa dunia mjini Moscow akiwa na medali tatu za dhahabu, licha ya kuhitaji kuwa katika hali yake ya juu kabisa ya kasi.
Bolt alikamisha mavuno ya medali tatu za dhahabu katika mbio za mita 100, 200 na mbio za mita 400 kupokezana vijiti, na kuwa mwanariadha aliyefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika historia ya mashindano hayo ya dunia.
Kama ilivyokuwa kwa Bolt na Fraser-Price , Mo Farah aling'ara pia. Raia huyo wa Uingereza alithibitisha nafasi yake kuwa miongoni mwa wakimbiaji wa masafa marefu akirejea ushindi wake wa mbio za mita 5,000 na 10,000.
Farah alipata medali yake ya dhahabu katika mbio za mita 10,000 mwanzoni mwa mashindano hayo na kunyakua medali nyingine ya dhahabu siku sita baadaye katika mbio za mita 5,000.
Urusi ilikuwa mshindi wa juma la medali ikiipiku Marekani , kwa kunyakua medali saba za dhahabu kwa sita za Marekani.
Wanawake wa Ethiopia waling'ara katika mashindano haya ambapo Tirunesh Dibaba alijinyakulia medali ya dhahabu katika mbio za mita 10,000 na mwezake Meseret Defar alishinda mbio za mita 5,000.
Udhibiti Kenya wa mbio za kuruka vikwazo uliendelea kwa kupitia Ezekiel Kemboi. Nae Milcah Chemos Cheywa alishinda katika mbio za wanawake.
Steven Kiprotich wa Uganda alionesha kuwa ushindi wake wa olimpiki haukuwa wa kubahatisha baada ya kuwaweka kando Waethiopia.
Na hatimaye ni taarifa za mwanariadha mlemavu wa Afrika kusini Oscar Pistorius kwamba ameshtakiwa leo kwa kosa la kuua kwa kukusudia na kumiliki silaha kinyume na sheria kwa kumpiga risasi na kumuua mpenzi wake katika siku kuu ya Wapendaoa.
Mahakama ya mjini Pretoria leo imepanga Machi 3 kuwa ni siku itakayosikilizwa kesi ya Pistorius, ambaye amesema alimpiga risasi mpenzi wake Reeva teenkamp kwa makosa, akifikiri kuwa ni mwizi.
Mwandishi: Sekione Kitojo/APE/AFPE/DPAE/RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef