Bundesliga yarejea kwa kishindo
21 Agosti 2017Bao lao lilipatikana mapema katika kipindi cha pili wakati Nico Elvedi alifunga bao safi baada ya kupokea krosi kutoka kwa Ibrahima Traore. Matthias Ginter ni beki wa Gladbach "michuano ya dabi huwa maalum kwa mashabiki na wale wote wanaohusika na klabu. Kuna tofauti. Iwe ni mtu kuja ofisini kesho na kuweka bendera ya Cologne au Gladbach. Hii kawaida huwa michezo maalum na mazingira mazuri na ndio maana tuna furaha kubwa kuwa tumeshinda.
Katika mechi nyingine ya jana, Freiburg na Eintracht Frankfurt zilianza msimu kwa kutoka sare ya bila kufungana. Freiburg ilifunga bao katika kipindi cha kwanza, lakini mfumo wa kutumia video ulifuta bao la Tim Kleindienst baada ya kugundua kuwa mchezaji mwenzake alikuwa ameotea wakati bao hilo lilifungwa.
Mfumo huo wa VAR unafanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza katika ligi ya Ujerumani msimu huu. Ulianza kutumika Ijumaa na Bayern walinufaika kwa kupewa penalti ambayo Robert Lewandowski alifunga na kuwapa mabingwa hao watetezi ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Bayer Leverkusen katika mechi ya ufunguzi.
Kevin-Prince Boateng arejea Bundesliga
Kiungo wa Ghana Kevin-Prince Boateng alicheza mechi yake ya kwanza na Eintracht Frankfurt baada ya kuwa nje ya Bundesliga kwa miaka miwili alipotupwa nje ya kikosi cha Schalke. Na hapa anauzungumzia mchuano wa jana. "Nadhani tulionyesha mchezo mzuri. Tulikuwa imara kabisa katika ulinzi na ni bao pekee lililokosekana. Tulikuwa na nafasi mbili nzuri ambazo bahati mbaya hatukuzitumia vyema na hivyo hatujaweza kuchukua pointi tatu leo. Lakini nnaridhishwa na mchezo wa timu. Hatujaweza kuacha chochote nyuma.
Boateng mwenye umri wa miaka 30 alikamilisha uhamisho wa haraka haraka kwa kusaini mkataba wa miaka mitatu na Frankfurt baada ya kuihama klabu ya Las Palmas ya Uhispania akitaja sababu za kibibafsi.
Katika mechi za Jumamosi, Borussia Dortmund iliizidi nguvu VfL Wolfsburg kwa kuilaza tatu bila. Kocha mpya Peter Bosz aliahidi kandanda la kuvutia, la kushambulia na timu yake, ambayo ilimaliza katika nafasi ya tatu msimu uliopita iliidhihirisha hilo. Mabao ya BVB yalifungwa na Christian Pulisic, Marc Bartra na Pierre-Emerick Aubameyang. Msikilize kocha Bosz "unapaswa kuridhika wakati umeshinda mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Wolfsburg na umekuwa na mchezo mzuri. Sehemu kubwa ya mchezo ilikuwa nzuri sana, hatukufungwa bao, lazima uridhike.
Ousmane Dembele anaondoka au anabaki?
Na wakati BVB walishinda bila ya nyota wao Ousmane Dembele, suali ni kuwa je, anaondoka au atabaki? Afisa mkuu mtendaji wa Dortmund Hans-Joachim Watzke anasema klabu hiyo haina nia ya kulegeza msimamo wake kuhusiana na Dembele anayesakwa na Barcelona. Hiyo ina maana kuwa hatua ya kumwondoa Dembele kwenye shughuli za kikosi cha kwanza baada ya kukosa kufika mazoezini itaendelea kutekelezwa. Na Dortmund haitapunguza kiasi cha fedha wanachotaka kupewa kwa ajili ya kumuuza nyota huyo mwenye umri wa miaka 20.
Kwingineko, Schalke ilianza msimu kwa ushindi wa mabao mawili kwa bila dhidi ya RB Leipzig ambao walimaliza wa pili msimu uliopita. Na kwa matokeo hayo, inaonekana kuwa kocha wao chipukizi Domenico Tedesco amejiandaa kuirejesha klabu hiyo katika kiwango cha juu. Katika matokeo mengine, Hoffenheim walipata ushindi wa moja bila dhidi ya Werder Bremen, Hertha Berlin ikaifunga Stuttgart mbili sifuri. Vladimir Darida ni kiungo wa HSC "nadhani ilikuwa muhimu sana kwetu kujiamini baada ya kupata pointi tatu katika mechi ya kwanza ya msimu. Ni mwanzo mzuri, lakini msimu bado ni mrefu na lazima tuweze kucheza katika kila mtangane kama tilivyocheza leo".
Hanover iliishinda Mainz moja bila wakati Hamburg ambayo ilinusurika kushushwa daraja msimu uliopita, iliifunga Ausburg moja bila, huyu hapa kiungo wa Hamburg, Aaron Hunt. "Unaweza kufikiria nini kingetokea hapa tena kama hatungekuwa tumeshinda. ndio maana timu imekuwa bora zaidi kwa sababu inacheza kwa pamoja tena. Lazima niisifie timu. Imejaribu kucheza vizuri kabisa kwa kujituma. Tumepambana kwelikweli leo na nadhani mwishowe tulistahili kupata ushindi.
Lakini ushindi huo ulikuwa na gharama yake baada ya mfungaji wa bao hilo Nicolai Mueller kuumia wakati akishangilia goli lake na sasa atakuwa mkekani kwa karibu miezi saba
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman