1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga yarejea uwanjani ; Bayern yaendeleza ubabe

25 Januari 2014

Bayern Munich imeanza duru ya pili ya Bundesliga kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Borussia Moenchengladbach jana Ijumaa baada ya mapumziko ya wiki tano ya majira ya baridi.

https://p.dw.com/p/1AwzH
Bundesliga FC Bayern München Borussia Mönchengladbach Sport Deutschland
Mario Goetze wa Bayern akituliza boliPicha: Getty Images

Mario Goetze alifunga bao la kuongoza katika dakika ya saba ya mchezo, wakati walinzi wa Moenchengladbach walipomuacha bila ulinzi na kuupachika mpira wavuni , kabla ya Thomas Mueller kukamilisha ushindi wa bayern kutokana na mkwaju wa penalti katika dakika ya 54.

Granit Xhaka wa moenchengladbach alitumia mkono kuusimamisha mpira katika mtafaruku golini na ndipo refa akaamua mkwaju wa penalti kwa Bayern.

Bundesliga FC Bayern München Borussia Mönchengladbach Sport Deutschland
Pambano kati ya Bayern dhidi ya MoenchengladbachPicha: Getty Images

Moenchengladbach ambayo ilikuwa haijafungwa nyumbani msimu huu, ilifanikiwa tu mara mbili kugonga mwamba wa goli la Bayern , wakati Max Kruse na patrick Herrmann waliopojaribu bahati yao dhidi ya kipa wa Bayern Manuel Neuer.

Bayern bado ni wababe

Bayern imeendeleza ubabe wa kutofungwa katika Bundesliga kwa michezo 42 na sasa imepanua mwanya wa uongozi hadi point 10 ikifuatiwa na Bayer Leverkusen ambayo inacheza leo jioni dhidi ya Freiburg.

Mabingwa hao hata hivyo wana mchezo mmoja zaidi ambapo watacheza dhidi ya Stuttgart siku ya Jumatano ili kutimiza michezo 18 ya ligi ya Ujerumani Bundesliga hadi sasa.

Iwapo tutacheza kama tulivyocheza leo tutakuwa mabingwa wa Ujerumani, amesema rais wa Bayern Uli Hoeness.

Zum Thema - Uli Hoeneß muss vor Gericht
Rais wa Bayern Uli HoenessPicha: Reuters/Michaela Rehle

Mshambuliaji mashuhuri wa Bayern Mario Mandzukic hakuwamo katika kikosi hicho jana. Mkurugenzi wa sporti wa Bayern Munich Matthias Sammer amesema kabla ya mchezo huo kuwa mshambuliaji huyo kutoka Croatia hajafanya mazowezi vya kutosha.

Hakutaka kusema hata hivyo iwapo usajili wa Robert Lewandowski kutoka Borussia Dortmund kwa ajili ya msimu ujao una athari yoyote katika hilo.

Michezo mingine hii leo ni kati ya nuremberg dhidi ya Hoffenheim, Borussia Dortmund inapimana nguvu na FC Augsburg, na VFB Stuttgart inaikaribisha Mainz. Wolfsburg ina miadi na Hannover 96 wakati Eintracht Frankfurt ni wenyeji wa Hertha BSC Berlin.

Kesho(26.01.2014) ni zamu ya Werder Bremen itakayotiana kifuani na Eintracht Braunschweig na Schalke 04 iko ugenini dhidi ya Hamburg SV.

Bundesliga 1899 Hoffenheim Borussia Dortmund
Wachezaji wa Borussia Dortmund wakipongezana baada ya kupata baoPicha: Reuters

Wakati huo huo Lukas Podolski aliweka mpira wavuni katika kipindi cha kwanza jana na kuisaidia Arsenal kuirarua Coventry ya daraja la tatu kwa mabao 4-0 katika mchezo wa duru ya nne ya kombe la FA.

Arsenal yapeta

Katika mchezo ambao Arsenal iliutawala toka mwanzo hadi mwisho, Podolski aliwainua mashabiki wa Arsenal katika dakika ya 15 kwa kufunga bao safi baada ya kumegewa pasi safi na Mesut Ozil. Aliongeza bao la pili kwa kichwa kunako dakika ya 27 ya mchezo.

Lukas Podolski
Mshambuliaji wa Arsenal Lukas PodolskiPicha: Bongarts/Getty Images

Katika mchezo mwingine wa kombe la FA jana Ijumaa , Nottingham Forest ilitoka sare ya bila kufungana na Preston.

Wakati huo huo kocha wa zamani wa Manchester United Alex Ferguson ameteuliwa kuwa kocha balozi wa shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA. Sir Alex atakuwa mwenyekiti wa jopo la makocha wateule ambao wanakutana kila mwaka, amesema rais wa UEFA Michel Platini.

Mwandishi: Sekione Kitojo

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman