Bundesliga yarejea uwanjani
17 Januari 2013Mengi yanatarajiwa katika kipindi hiki baada ya awamu iliyopita kukumbwa na timuatimua ya makocha kutokana na matokeo mabaya ya baadhi ya vilabu vinavyoshiriki kinyang'anyiro hicho.
Ijumaa (tarehe 18 Januari) Bundesliga itaanza kwa klabu ya soka ya Schalke kushikana mashati na Hannover katika mechi itakayochezwa usiku saa moja na nusu kwa saa za hapa Ujerumani ambazo ni sawa na saa 3 na nusu Afrika ya Mashariki.
Vinara wa Bundesliga, Bayern Munich, wataumana na Greuther Fuerth Jumamosi (19.1.2013) huku wakiwa na matumaini ya kuwa na mwanzo mzuri wa awamu hii.
Matumaini ya Bayern Munich
Kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes, mwenye umri wa miaka 67 sasa, ana mategemeo ya kustaafu vyema hapo mwenzi Mei mwaka huu kwa kukiwezesha kikosi chake kunyakua taji la Bundesliga msimu huu.
Heynckes atarithiwa na mkufunzi machachari wa kabumbu la kimataifa kutoka klabu ya Barcelona, Pep Guardiola, ambaye tayari Bayern Munich imeshaweka wazi kuwa kocha huyo ni wao katika msimu ujao.
Wana Bavaria hao wenye jumla ya pointi 42, wako kileleni kwa tofauti ya pointi tisa kutoka nafasi ya pili inayoshikiliwa na Bayer Leverkusen yenye pointi 33 huku mabingwa watetezi wa taji la Bundesliga msimu uliopita, Borussia Dortmund, wakishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 30.
Leverkusen, ambao walimaliza ngwe iliyopita mwezi Desemba mwaka jana kwa kushinda mechi tano kati ya sita walizocheza, kesho watachuana na Eintracht Frankfurt wanaoshikilia nafasi ya nne. Frankfurt kama walivyo Dortmund nao pia wana jumla ya pointi 30 huku taarifa zikisema kuwa sasa mshambuliaji wao machachari, Stefan Kiessling, akiwa ameiva vyema kwa ajili ya ngwe hii.
Ndoto za Dortmund kutetea taji lake
Kwa upande wao Borussia Dortmund wanaopigana kufa na kupona kulinda taji la Bundesliga Jumamosi (19.1.2013) watasafiri kwenda kukutana na Werder Bremen katika mchezo ambao unategemewa kuweza kuinua matumaini ya wapenzi wa mabingwa hao watetezi.
Tunafahamu mabadiliko kadhaa yalifanyika katika Bundesliga kabla ya mapumziko ya majira ya baridi ambapo tumeshuhudia baadhi ya vilabu vikiwatimua makocha wake kutokana na matokeo mabaya katika kinyang'anyiro hicho.
Na katika ngwe hii kila timu imetangaza kufanya maajabu ya kuwania taji. Bila shaka kuna mengi ya kushuhudiwa katika Bundeliga hasa wakati huu wachezaji wamerudi na nguvu mpya kabisa baada ya mapumziko.
Mechi zingine zitakazochezwa Jumamosi ni Mainz ambao watachuana na Freiburg, Wolfsburg wataumana na Stuttgart na Hoffeinheim itakwaana na Moenchengladbach.Jumapili kutakuwa na michezo miwili ambapo Nuremberg itacheza na Hamburg wakati Fortuna Dusseldorf itakutana na Augsburg.
Mwandishi: Stumai George/Dpa/Reuters/Afp
Mhariri: Josephat Charo