1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mainz inapambana na mabingwa wa Bundesliga, Bayern Munich.

24 Septemba 2010

Baada ya kuifunga Köln 2-0, Mainz inatarajiwa kukutana na Bayern Munich.

https://p.dw.com/p/PM8o
Wakufunzi wa Bayern na Mainz, Louis Van Gaal na Thomas Tuchel.Picha: picture alliance/dpa

Bila shaka hadithi inayoendelea kusimuliwa wiki hii katika mashindano ya Bundesliga ni ushindi wa Mainz dhidi Köln wa mabao 2-0, ulioipa timu hiyo, kwa mara ya tano, ushindi katika michuano yake na pia uongozi wa pointi tano mbele ya Hoffenheim  iliyoshindwa mabao 2-1 nyumbani na mabingwa Bayern Munich.

Inaonekana Bahati imeilalia Mainz msimu huu ambapo ni mara ya kwanza inaongoza mashindano hayo ya Bundesliga kwa wingi wa pointi.

Hata hivyo, mchezo wake dhidi Köln haukuwa wa kusisimua ikilinganishwa na michuano yake mingine ya hapo awali.

Uamuzi wa kocha Thomas Tuchel kumuingiza Lewis Holtby kunako dakika 64 ya awamu ya pili ya mchuano huo, kulifua madafu, maana asante ya Holtby kupewa fursa hiyo, ilidhirika kupitia mikwaju aliyoisukuma wavuni mwa Köln, la kwanza dakika 9 baada ya kuingia uwanjani na la pili katika dakika za lala salama.

Fussball 1. FSV Mainz 05 - 1. FC Koeln Lewis Holtby
Lewis Holtby wa timu ya Mainz.Picha: AP

Baada ya kudhirisha mlingoti chuma, huenda Mainz inapania katika uwanja wa Allianz kudhihirisha kuwa bendera yake pia ichuma, kwa kuihangaisha bingwa Bayern Munich.

Swali ni je itafaulu?

Kwa upande wake, mabingwa wa Bundesliga, Bayern Munich, wamejizatiti kuonyesha mchezo wa hali ya juu msimu huu na wanamkosa winga, Frank Ribery, kwa muda wa wiki nne zijazo kufuatia jeraha la mguu alilolipata wakati wa mchuano dhidi Hoffenheim.

Huku mholanzi Arjen Robben akiwa pia nje kutokana na jeraha, matumaini makuu ya Bayern ni kwa wananyota Bastian Schweinstieger na Thomas Mueller, kutekeleza mashambulizi mithili ya viwavi.

Msimu huu, Bayern chini ya ukufunzi wake Louis Van Gaal imeorodheshwa ya nane ikiwa na pointi nane, nyuma ya Mainz.

Kocha Van Gaal atakumbukwa kwa mchango wake wa kuipa ushindi mara mbili  timu hiyo kwenye mashindano hayo ya Bundesliga katika msimu wake wa kwanza na pia kombe la Ujerumani, na kwa kufanikiwa kuiongoza timu hiyo hadi katika fainali za champions league walikoshindwa na Intermilan 2-0.

Bayern inamatumaini makubwa kuwa kocha huyo anakaribia kutia saini mkataba wa mwaka mmoja zaidi wa kuifunza timu hiyo.

Mwandishi: Maryam Abdalla/ DPAE/AFPE

Mhariri : Miraji Othman