Bundesliga:Dortmund kuumana Hannover 96
1 Aprili 2011Polisi wa Ujerumani hapo siku ya Jumatano walitoa taarifa ya kwamba wamefanikiwa kuzima jaribio la kutaka kufanyika kwa shambulio kwenye uwanja huo.
Dortmund mnamo wiki mbili zilizopita mwanya wake wa uongozi ulipunguzwa hadi pointi saba kufuatia sare ya bao 1-1 na Mainz huku wanaowanyatia kileleni Bayer Leverkusen wakipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Schalke 04.
Hannover yenyewe inakamata nafasi ya tatu na ni timu iliyoonesha mchezo mzuri katika hatua hii ya lala salama ya Bundesliga.
Timu hiyo sasa inatishia nafasi ya mabingwa watetezi Bayern Munich kupata nafasi ya kucheza katika ligi ya mabingwa barani Ulaya yaani Champions League. Munich wako katika nafasi ya nne pointi mbili nyuma ya Hannover yenye pointi 50, na Jumamosi hii wanakumbana na timu inayokamata mkia Borussia Moenchengladbach.
Fainali ya Champions League msimu ujao itafanyika mjini Munich na Bayern wanataka kucheza fainali hiyo. Kutokana na hilo, Rais wa Bayern Munich Uli Hoeness amenukuliwa akisema kuwa atakuwa mshabiki mkubwa wa Dortmund akitaka iifunge Hannover na wao waifunge Moechengladbach na hivyo kuchupa hadi katika nafasi ya tatu.
Lakini kocha wa Dortmund Jürgen Klopp, alipoulizwa kuhusiana na shabiki huyo mpya hii leo, alisema
´´Mimi pia nimesoma katika magazeti kuwa katika mechi hii ya leo Uli Hoeness atakuwa mshabiki wetu. Ni lazima tushinde hata kama hatakuwa upande wetu´´
Nayo Bayer Leverkusen watakuwa ugenini kuumana na timu inayotapia kushuka daraja Kaiserslautern. Leverkusen inawania kupata pointi zaidi kwa mawili kwanza kuzidi kuimarisha tumaini lake la kutwaa ubingwa na pili kujihakikishia zaidi nafasi ya kucheza kwenye Champions League. Kocha wa timu hiyo Jupp Heynckes ambaye msimu ujao atakuwa na Bayern Munich, alisema ataka kuhakikisha wanapata moja kati ya nafasi hizo.
´´Nitakuwa imara hadi mwisho wa msimu. Maana yake ni kwamba nataka tuweze kufanikiwa moja kwa moja kufuzu kwa ligi ya mabingwa´´
Mechi nyingine za Bundesliga Jumamosi hii zitashuhudia Werder Bremen wakiwaalika uwanjani Stuttgart, timu ambazo zinahitaji ushindi ili kuzidi kulikwepa shimo la kushuka daraja. Mainz watakuwa nyumbani kuumana na Freiburg, huku Hoffenheim wakiwaalika uwanjani Hamburg.
Mwandishi:Aboubakary Liong/Reuters/ZPR
Mhariri:Josephat Charo