Bundesliga:Dortmund yaukaribia ufalme
18 Aprili 2011Kwa upande wao Bayer Leverkusen katika matokeo yanayowapa wasiwasi washabiki ilikubali kipigo cha mabao 5-1 kutoka Bayern Munich.Kipigo hicho kimeipunguza kasi Leverkusen kuweza kuwafikia Dortmund kwani sasa mwanya uliyopo ni pointi nane.
Ikumbukwe ya kwamba kocha wa Leverkusen Jupp Heynckes msimu ujayo anajiunga na Bayern Munich ambayo inapigana kufa na kupona kuhakikisha inapata nafasi ya tatu na kucheza katika Champions League msimu ujayo.
Ushindi huo umeifanya ichupe katika nafasi ya tatu kufuatia suluhu ambayo Hannover 96 iliipata mbele ya Hamburg.
Kutokana na mazingira hayo washabiki wengi wa soka hapa wanasema wanasema kocha huyo wa Leverkusen alikula njama, kwani hawezi kuifundisha timu ambayo itakuwa haishiriki katika ligi hiyo ya mabingwa barani Ulaya.
Hata hivyo akijitetea kocha huyo wa Leverkusen Heynckes alisema kuwa ni ugumu wa kisaikolojia uliyotawala kabla ya kuanza kwa mechi ndiyo uliyopelekea kipigo hicho.
Kwa upande wao Borussia Dortmund tayari hivi sasa wanaota kuwa wamekwishatawazwa kuwa mabingwa na mara baada ya filimbi ya mwisho hapo jana washabiki na wachezaji walishangilia kama vile wamekwishautwaa.
Katika mechi nyingine FC Cologne ilipata kipingo kingine, tena katika uwanja wake wa nyumbani mjini Cologne kwa kuchapwa mabao 3-1 na Stuttgart, na hivyo kuendelea kubakia katika nafasi ya 12 na Stuttgart katika nafasi ya 14.
Werder Bremen ilitoshana ubavu na Schalke 04 kwa kufungana bao 1-1 huku,Wolfsburg inayopambana kukwepa kushuka daraja ikitoka sare ya mabao 2-2 na St Pauli.
Kwa upande wa watia mabao Mario Gomez wa Bayern Munich sasa anaongoza akiwa na mabao 22 baada ya hapo jana kuzifumania nyavu mara nne pekee yake kwenye ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Bayer Leverkusen.Nafasi ya pili inashikiliwa na Papiss Cisse wa Freiburg mwenye mabao 20.
Mtayarishaji:Aboubakary Liongo/ZPR/Reuters/DPA
Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman