1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge Afrika Kusini lapiga kura kusitisha uhusiano na Israel

22 Novemba 2023

Wabunge nchini Afrika Kusini wamepiga kura ya kuufunga ubalozi wa Israel mjini Pretoria.

https://p.dw.com/p/4ZHum
Afrika Kusini | Wanaharakati wanaounga mkono Palestine mjini Cape Town
Wanaharakati wa Afrika Kusini wakiandamana kuonyesha uungwaji mkono wao kwa PalestinePicha: Gianluigi Guercia/AFP/Getty Images

Wabunge pia wameihimiza mamlaka nchini humo kukata kwa muda uhusiano wa kidiplomasia na Israel hadi makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza yatakapoafikiwa.

Siku ya Jumatatu, Israel ilimuita nyumbani balozi wake nchini Afrika Kusini kwa kile walichokiita mashauriano kabla ya wabunge kupiga kura.

Kura hiyo iliyoitishwa na chama cha upinzani, iliungwa mkono na Rais Cyril Ramaphosa wa chama tawala cha ANC. Serikali ya Ramaphosa itakuwa na uamuzi wa mwisho iwapo hatua zilizochukuliwa na bunge zitatekelezwa.

Mapema jana, Rais Cyril Ramaphosa aliandaa mkutano kwa njia ya mtandao na viongozi wenzake wa BRICS kuujadili mzozo kati ya Israel na Kundi la Hamas.

Wakati wa mkutano huo, kiongozi huyo wa Afrika Kusini alikosoa hatua za serikali ya Israel katika mzozo wake na Hamas. Aliishtumu Israel kwa uhalifu wa kivita na kutekeleza "mauaji ya halaiki" katika ukanda wa Gaza.

Israel hata hivyo imekanusha shutma hizo.