1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Tanzania lajadili visa vya utekaji na watu kupotea

Deo Kaji Makomba, Dodoma6 Mei 2019

Mbunge Peter Msigwa wa CHADEMA amesema kuwa matukio ya mauaji, utekaji na watu kupotea yamekuwa yakiendelea nchini humu na hivyo kuendelea kuzua hofu miongoni mwa Watanzania.

https://p.dw.com/p/3Hz9w
Tansania Parlament Dodoma - Parlamentsvorsitzende mit Philip Mpango und Premierminister Kassim Majaliwa
Picha: DW/S. Khamis

Sakata la matukio ya mauaji, utekaji na watu kupotea huko nchini Tanzania leo limetua bungeni baada ya mbunge Peter Msigwa kuomba hoja ya dharura ili bunge liweze kujadili matukio hayo ambapo kulingana na mbunge huyo yamekuwa yakiendelea na hivi karibuni mtu mmoja aliyejulikana kwa jina Mduda Nyagali ametekwa na watu wasiojulikana huko wilayani Mbozi mkoani Songwe huku jeshi la polisi likilalamikiwa kutochukua hatua yoyote.

Akizungumza bungeni mjini Dodoma, Mbunge Peter Msigwa wa CHADEMA amesema kuwa matukio ya mauaji, utekaji na watu kupotea yamekuwa yakiendelea nchini humo na hivyo kuendelea kuzua hofu miongoni mwa Watanzania huku serikali kupitia mamlaka zake husika likiwemo jeshi la Polisi kushindwa kuyatolea taarifa matukio hayo yanayokwenda kinyume na haki za binadamu na hivyo kulitaka bunge lijadili kwa dharura suala hilo:

Vyombo vya usalama vimekana madai kuwa hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya watu kupotea.
Vyombo vya usalama vimekana madai kuwa hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya watu kupotea.Picha: DW/E.Boniphace

Lakini wizara ya mambo ya ndani ya nchi, kupitia naibu waziri wake Hamadi Yusufu Masauni, imesema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimekuwa vikifanya kazi ili kukabiliana na matendo hayo huku akikanusha kuwa sio kweli kwamba hakuna hatua zozote ambazo zimechukuliwa na serikali.

Naibu waziri huyo mwenye dhamana ya usalama wa raia na mali zao alikwenda umbali wa kuliamuru jeshi la polisi kumuhoji mbunge Peter Msigwa ili athibitishe kauli yake aliyoitoa:
 

Katika siku za hivi karibuni, matukio ya wale waitwao watu wasiojulikana kufanya mauaji na kuwateka raia, wasanii, wanasiasa na wafanyabiashara yamekuwa yakiendelea nchini humu na hivyo kuendelea kuzua taharuki miongoni mwa wananchi.

Tukio la karibuni kabisa ni la juzi Jumamosi, ambapo kijana mmoja anayejulikana kwa jina la Mdude Nyagali alitekwa mkoani Songwe, na hadi hivi sasa hajulikani alipo.