Bunge la EU lakaa kimya kuwakumbuka wahanga wa Oktoba 7
8 Oktoba 2024Wabunge wa Umoja wa Ulaya jana Jumatatu walikaa kimya kwa dakika moja ili kuwakumbuka wahanga wa shambulio la Oktoba 7 lililofanywa na kundi la Hamas dhidi ya Israel huku Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akiapa kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi.
Von der Leyen amekosoa kile alichokitaja kama ongezeko la kutisha la chuki dhidi ya Wayahudi barani Ulaya wakati alipohudhuria hafla ya kumbukumbu ya shambulio la Oktoba 7 iliofanyika mjini Brussels.
Soma pia: Von der Leyen aizuru Ukraine kujadili usalama wa nishati
Amesema kuwa chuki dhidi ya Wayahudi ni tishio kwa demokrasia na kufananisha chuki hiyo kama saratani inayotishia misingi ya Umoja wa Ulaya.
Kulingana na takwimu za shirika la habari la AFP, shambulio la Hamas katika ardhi ya Israel lilisababisha vifo vya watu 1,205 wengi wao wakiwa raia.
Maadhimisho ya kumbukumbu ya shambulio la Oktoba 7 yamefanyika wakati Israel inaendeleza oparesheni ya kijeshi katika ukanda wa Gaza na kwa upande mwengine, jeshi la nchi hiyo linapambana na kundi la Hezbollah nchini Lebanon.