1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Uturuki laidhinisha utumaji wanajeshi Libya

Sylvia Mwehozi
2 Januari 2020

Wabunge wa Uturuki wameidhinisha uingiliaji wa kijeshi nchini Libya kwa kupiga kura ya kuunga mkono kutumwa wanajeshi wake katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini kwa kipindi cha mwaka mmoja.

https://p.dw.com/p/3VbxA
Türkei Parlament Ankara
Picha: Getty Images/AFP/A. Altan

Mswada wa kuwapeleka wanajeshi nchini Libya umeidhinishwa kwa jumla ya kura 325 za ndio dhidi ya 184 za hapana. Hoja hiyo ilitarajiwa kupitishwa kwa urahisi kwa sababu chama cha rais Recep Tayyip Erdogan cha Haki na maendeleo - AKP na mshirika wake chama cha harakati za kitaifa MHP, vina wingi wa viti bungeni. Kikao cha dharura kiliitishwa kujadili hoja hiyo ambayo itairuhusu serikali kuamua muda na kiwango cha wanjeshi watakaotumwa Libya.

Serikali ya mjini Tripoli ya waziri mkuu wa Libya Fayez Sarraj imekabiliwa na mashambulizi ya utawala hasimu wa kamanda Khalifa Haftar katika eneo la mashariki ya nchi. Mashambulizi hayo yametishia kuitumbukiza Libya katika machafuko zaidi ya baada ya mwaka 2011 yaliyomuondoa kiongozi wa muda mrefu Moamar Gadaffi.

Türkei Istanbul | Libyens Premierminister al-Sarraj trifft Erdogan
Rais Recep Tayyip akiwa na rais wa serikali ya Libya Fayez al SarrajPicha: picture-alliance/AP Photo/Turkish Presidency

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema mwezi uliopita kwamba Sarraj aliiomba Uturuki kuwatuma wanajeshi wake, baada ya viongozi hao wawili kutia saini makubaliano yanayoiruhusu Ankara kuwatuma wataalamu wa kijeshi nchini Libya. Makubaliano hayo, sambamba na makubaliano mengine ya mipaka ya majini baina ya Uturuki na Libya, yamezusha hofu katika ukanda huo na kwingineko.

Ankara inasema utumaji wa wanajeshi ni muhimu kwa Uturuki katika kuyalinda maslahi yake nchini Libya na eneo la mashariki mwa Mediterenia, ambako imejikuta ikitengwa zaidi na Ugiriki, Cyprus, Misri na Israel ambazo zimetengeneza ukanda thabiti wa kiuchumi kwa ajili ya kupisha uchimbaji gesi na mafuta.

Makamu wa rais wa Uturuki Fuat Oktay ameliambia shirika la habari la nchi hiyo Anadolu kwamba Uturuki itatuma wanajeshi wa kutosha pindi panapokuwa na mahitaji. Lakini pia alisisitiza kwamba serikali yake haitotuma wanajeshi Libya endapo kiongozi hasimu atasimamisha mashambulizi yake. "Kama upande mwingine utachukua mwelekeo mwingine na kusema sawa tunajiondoa, tunarudi nyuma, basi kwanini sisi tuingie", alisema makamu wa rais.

Libyen Kämpfe | Kämpfer von General Khalifa Haftar
Wanajeshi tiifu kwa kamanda HaftarPicha: Getty Images/AFP/A. Doma

Chama kikuu cha upinzani cha Uturuki CHP, kilisema awali kwamba kitaipinga hoja hiyo kwasababu utumaji wanajeshi utaitumbukiza Uturukikatika mzozo mwingine na kuifanya kuwa sehemu ya umwagaji damu wa Waislamu.

Kiongozi wake Kemal Kilicdaroglu alitoa wito kwa serikali ya Uturuki kufanyia kazi uanzishwaji wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulind amani libya. Chama kingine cha upinzani kilicho na mrengo wa kati nacho kilisema awali kwamba kisingeunga mkono hoja hiyo. Hata hivyo chama tawala cha Erdogan kinashirikiana na chama cha kitaifa na vyote viwili vina kura ya kutosha ya kuidhinisha hoja hiyo.

Mapambano mjini Tripoli yalishika kasi katika wiki za hivi karibuni bada ya kamanda Haftar kutangaza mapambano ya mwisho kwa ajili ya mji mkuu Tripoli. Haftar anaungwa mkono na Umoja wa falme za Kiarabu na Misri pamoja na Ufaransa na Urusi wakati serikali ya mjini Tripoli ikipokea misaada kutoka Uturuki, Qatar na Italia.