Bunge laridhia kuchelewesha Brexit
15 Machi 2019Bunge la Uingereza limepiga kura kukubali kuongezewa muda wa kujiondoa kwa nchi hiyo kutoka kwenye Umoja wa Ulaya kwa kura 412 zilizokubali dhidi ya kura 202 zilizotaaa. Kabla ya hapo Uingereza ilipaswa kuondoka kisheria kutoka Umoja wa Ulaya Machi 29.
Lakini sababu bunge hilo lilikataa mpango wa Waziri Mkuu Theresa May siku ya Jumanne, ilibidi waombe kuongeza muda wa mchakato huo.
Kuongezwa huko muda inabidi pia kukubaliwa na nchi 27 za Umoja wa Ulaya katika mkutano wao wa kilele Machi 21 na 22.
Wahafidhina na uwezekano wa Brexit ya mapema
Anayeonekana kuwa makamu wa Waziri Mkuu wa Uingereza, David Lidington, ameliambia shirika la habari la Uingereza, BBC kwamba bado nchi hiyo inataka kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya kwa kufata utaratibu maalum na bado ina mpango wa kutoka Machi 29, labda kama kutakuwa na mpango mbadala.
Lidington aliongeza kusema kuwa, ana matumaini bado wanaweza kutoka kwenye Umoja wa Ulaya hivi karibuni kwa kufuata utaratibu, lakini hiyo inategea kama bunge litayapitisha hayo makubaliano ya kujitoa na kutekeleza sheria zitakazofuata kabla ya na kupitisha mkataba huo wa kujitoa.
Amesema mpaka mwisho wa Machi, inabidi kuwe na mbadala, sio tu maazimio ya bunge, bali wanapaswa kuwa na mapendekezo pamoja na utatuzi ambao utawezesha kuwa na urefushwaji bila ya mgongano siku ya Machi 29.
Labour wataka kura ya pili ya maoni
Kwa upande mwingine, kiongozi wa chama cha Labour, Jeremy Corbin, amesema Theresa May inabidi akubali kwamba mpango wake wa kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya hauwezekani tena na pia kujiondoa kutoka umoja huo bila makubaliano pia haiwezekani.
Hivyo Corbin anaunga mkono kura ya pili ya maoni kwa Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya kama njia mbadala ya kuondoka katika mgogoro wa Brexit.
Aliyazungumza hayo baada ya bunge la Uingereza kupiga kura ya kuongeza muda wa kujiondoa, ingawa bunge hilo limekataa kura ya pili ya maoni kuhusu Brexit.
Mwandishi: Harrison Mwilima/RTRE1/ APE
Mhariri: Grace Patricia Kabogo