1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge Uganda laanza kujadili ukomo wa umri wa rais

Lubega Emmanuel18 Desemba 2017

Usalama uliimarishwa katika maeneo yanayozunguka bunge la Uganda wakati bunge hilo likianza kujadili ripoti kuhusu muswada wa kuondoa ukomo wa umri wa rais katika katiba ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/2paUW
Uganda Parlament Debatte über Alter für Präsidialamt
Bunge la Uganda likikutana kujadili muswada wa mabadiliko ya katiba kuondoa kipengele cha ukomo wa umri wa rais.Picha: DW/L. Emmanuel

Awali wabunge wa upinzani waliondoka kwa pamoja kwenye kikao cha alasiri wakipinga na kushtumu kile walichodai kuwa ukiukwaji mkubwa wa sheria na kanuni za utawala wa bunge na taifa kwa jumla. Hatua hiyo ilifutia uamuzi wa spika wa bunge Rebecca Kadaga kuwasimamisha wenzao sita kwa vikao saba kwa madai ya utovu wa nidham.

Kiongozi wa upinzani Winnie Kizza aliwaongoza wabunge wanaopinga kupitishwa kwa mswaada wa kuondoa ukomo wa umri wa rais kuondoka kwenye kikao ambapo mwenyekiti wa kamati ya bunge ya sheria na masuala ya bunge Oboth Oboth alikuwa anaanza kusoma.

Kiongozi huyo amelezea kuwa alichukua maamuzi haya kupinga kile alichokitaja kuwa tabia ya kushangaza ya spika wa bunge Rebecca Kadaga kukiuka kanuni za kuendesha shughuli za bunge na sheria za taifa na jumuiya ya afrika mashariki.

Tangu kwenye kikao cha asubuhi wabunge wanaopinga muswada utamuezesha rais Museveni kuwa rais wa maisha, walifanya kila juhudi kukosoa hatua ya kuwasilishwa kwa muswaada huo wakisema kuwa tayari walikuwa wamewasilisha shauri kwenye mahakama ya haki ya jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na ile ya katiba ya Uganda ili kuzuia mchakato huo kuendelea.

Uganda Kampala  Rebecca Kadaga Sprecherin Parlament
Spika wa Bunge la Uganda Rebecca Kadaga. Wapinzani wanamshtumu kwa ukiukaji wa kanuni za uendeshaji wa bunge.Picha: DW/Lubega Emmanuel

Walishangaa kwa nini spika Rebecca Kadaga aliidhinisha mjadala husika kuanza pamoja na kwamba alikuwa akionyesha upendeleo wakati wa kutoa fursa kwa wabunge kutamka lolote. Ni kwenye kikao hicho ndipo mabishano yalifululiza kati ya pande zote mbili, spika akalazimika kuahirisha kikao pamoja na kuwafukuza wabunge sita wasihudhurie vikao saba kuanzia kile cha alasiri.

Mnadhamu wa chama tawala Ruth Nankabirwa aliunga mkono maamuzi ya spika akielezea kuwa wabunge wa upinzaniu walikuwa wanafanya kila hila kuzuia muswaada huo kupitishwa, hivyo na wao waliamua kucheza mchezo wao.

Licha ya wenzao kuondoka kwenye ukumbi wa mijadala, wabunge wa chama tawala waliendelea na shughuli kwa mujibu wa ratiba. Walisikiliza kwa makini ripoti ya kamati ya bunge inayounga kubadlishwa kwa katiba.

Walipoondoka bungeni, wabunge wa upinzani waliwahutubia wandishi habari wakifafanua kuhusu maamuzi yao huku wakiwataka wananchi kuwaunga mkono kuhakikisha kwamba muswaada huo tete haupitishwi na wale wa chama tawala walio wengi.
 

Baada ya kikao cha wanahabari wabunge wa upinzani pamoja na wengine wa chama tawala wanaopinga muswada wa kuondoa ukomo wa rais ambao ni miaka 75, walirudi ukumbini kusikiliza ripoti ya wachache inayopinga ile ya wengie kama ilivyo ada ya kuwasilisha taarifa za kamati.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala

Mhariri: Mohammed Khelef