Bunge Uingereza lapitisha sheria ya kifo cha kusaidiwa
30 Novemba 2024Wabunge wa Uingereza wamepitisha kwa mara ya kwanza, mswada wa sheria ya kusaidia watu wazima walio na magonjwa yasiyotibika kukatisha maisha yao nchini England na Wales siku ya Ijumaa, kufuatia mjadala wenye hisia ambapo watu walitoa simulizi binafsi za kupoteza wapendwa wao na mateso.
Mswada huo wa kifo cha huruma uliidhinishwa na kura 330-275, ikiwa ni hatua ya kwanza kabla ya kuchunguzwa zaidi na kupigiwa kura ya mwisho. Kim Leadbeater, aliyekuwa mdhamini mkuu wa mswada huo, amesema lengo lake ni kuwapa watu wanaokufa chaguo kuhusu jinsi ya kufa.
Waungaji mkono walisema sheria hiyo ingetoa heshima kwa wanaokufa na kuzuia mateso, huku wapinzani wakihofia wazee na walemavu kulazimishwa kukatisha maisha yao ili kupunguza mzigo kwa familia.
Mswada huo unapendekeza watu wazima walio na chini ya miezi sita ya kuishi kuomba msaada wa kuhitimisha maisha yao, kwa kufuata tahadhari kadhaa.