Burkina Faso na Misri kupambana nusu fainali AFCON
1 Februari 2017Burkina Faso ilifanikiwa kutinga nusu fainali kwa kuibwaga Tunisia mabao 2-0 na Misri ikamfunga hasimu yake Morocco bao1-0. Mchezaji wa nafasi ya ulinzi wa Burkina faso Bakary Kone anayecheza katika kilabu ya Malaga katika ligi kuu ya uhispania La liga amesema wana matumaini makubwa ya kucheza fainali, huku Kocha wa Burkina Faso Mreno Paulo Duarte naye akisisitiza kwamba lengo lao ni kuiangusha Misri leo na kufika fainali . Burkina Faso itakuwa ikisaka nafasi nyengine ya kucheza fainali baada ya ile fainali ya 2013. Timu hizi zilikwisha kumtana katika nusu fainali miaka 21 iliopita pale Misri ilipoifunga Burkina Faso na hatimaye katika mechi ya fainali ikalitwaa kombe hilo la mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza. Kocha waburkina Faso Mreno Paulo Duarte amepokea salamu za kumtaka kila la kheri, kutoka kwa mwananchi mwenzake Kocha wa Manchester United Jose Mourinho. Duarte amemulezea Mourinho kuwa sio tu ni rafiki bali ni kama baba kwake.
Misri itakuwa tena uwanjani na mlinda mlango Essam el-Hadary mwenye umri wa miaka 44 na aliyeshinda mataji yote manne ya Kombe hilo akiwa na Misri, ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni miaka 19 iliopita. Ni vigumu kutabiri matokeo ya pambano hilo la leo na Mwalimu wa Misri Hector Cuper kutoka Argentina mwenye umri wa miaka 61 aliyewahi kuzifunza Valencia ya Uhispania na Inter Milan ya Italia, anasema licha ya majeruhi, wachezaji wake wako imara kuwakabili wapinzani wao.
Cameroon kumenyana na Ghana
Timu tatu zilizofanikiwa kuandika historia katika mashindano ya kandanda ya kombe la mataifa ya Afrika- Misri, Ghana na Cameroon zote zinaingia katika nusu fainali ya mashiondano ya safari hii, kila moja ikiwa imeshanyakuwa ubingwa mara nne. Baada ya nusu fainali kati ya Burkina Faso na Misri mjini Libreville, Alhamisi mjini Franceville itakuwa ni zamu ya Cameroon kutoana jasho na Ghana. Cameroon itakuwa inatafuta nafasi ya kumaliza kiu cha miaka 15 na Ghana ikiwania safari hii hatimaye kufuta machozi baada ya kulikaribia taji bila ya mafanikio kwa miaka 35.
Ghana itaingia uwanjani na kuuweka kando mkasa uliomkumba mlinda mlango wake Razak Brimah aliyetozwa faini ya dola 2,500 hapo jana kutokana na video aliyoiweka kwenye ukurasa wake wa Facebook. Video hiyo iliwalenga mashabiki waliomkosoa kwa baadhi ya matukio uwanjani. Razak aliwajibu kwa maneno haya "Ninyi na familia Zenu mnaweza kutokomea." Mchezaji huyo baadae aliomba radhi.Kuingia nusu fainali hiyo kesho, Ghana iliiadhibu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mabao 2-1 na Cameroon ikaibwaga Senegal moja ya timu zilizoekewa matumaini ya kufika fainali, kwa uamuzi wa matuta yaani mikwaju penalty, baada ya dakika 120 kumalizika bila ya kufungana. Fainali ya mashindano hayo itachezwa Jumapili.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri: Iddi Ssessanga