1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burkina Faso,Zambia na Ebola Magazetini

7 Novemba 2014

Hali nchini Burkina Faso ,Zambia na rais wa kwanza mzungu na kitisho cha maradhi hatari ya Ebola ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika wiki hii

https://p.dw.com/p/1DisI
Marais wa nchi tatu za Afrika Magharii,Dramani Mahma wa Ghana (3 kulia) akizungumza na wawakilishi wa Burkina faso pamoja na mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika Kodjo(kushoto) na rais wa Nigeria Jonathan Goodluck(3 kushoto) na rais wa Senegal Macky Sall (2 kulia)Picha: AFP/Getty Images/I. Sanogo

Tuanzie Afrika Magharibi ambako gazeti la "Die Tageszeitung la mjini Berlin linazungumzia juhudi za pande zote zinazohusika nchini Burkina Faso,kuanzia wanasiasa mpaka kufikia mashirika ya jamii kusaka ufumbuzi wa mzozo uliosababishwa na kutimuliwa madarakani rais Blaise Compaore baada ya kuitawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 27."Kipindi cha mpito kuambatana na katiba" ndio kichwa cha maneno cha die "Tageszeitung".Gazeti linazungumzia pia shinikizo la jumuia ya kimataifa na Umoja wa Afrika kuwataka wanajeshi wakabidhi haraka hatamu za uongozi kwa raia.Marais wa Ghana,Senegal na Nigeria sawa na mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika,waziri mkuu wa zamani wa Togo,Edem Kodjo,walikwenda Ouagadougou wiki hii kwajili hiyo.Ingawa luteni kanali Isaac Zida anaeiongoza nchi hiyo kwasasa,anaonyesha dalili za kutaka kukabidhi madaraka kwa raia,hata hivyo anasema muda wa wiki mbili uliowekwa na Umoja wa Afrika,haumhusu.Gazeti la die Tageszeitung linazungumzia pia utayarifu wa chama cha rais wa zamani Blaise Compaoré-Kongamano kwaajili ya demokrasia na maendeleo -CDP kushirikiana na pande zote zinazoheshimu demokrasia na taifa linalofuata sheria.

Mzambia weupe madarakani

Lilikuwa gazeti la mjini Munich la Süddeutsche Zeitung lililozungumzia kuhusu Zambia na kukabidhiwa kwa njia za kidemokrasia hatamu za muda za uongozi mzambia wa kwanza mwenye asili ya kizungu-Guy Scott."Mdomo Mpana" ndio kichwa cha maneno cha gazeti hilo ambalo baada ya kuandika kwamba wazee wake wanatokea Scottland na kwamba alisomea katika shule ya wasomi wa kizungu katika ile iliyokuwa zamani ikijulikana kama Rhodesia- leo,Zimbabwe , gazeti linasema Guy Scott amekabidhiwa wadhifa huo baada ya rais Michael Sata kuiaga dunia, kwasababu yeye ndie aliyekuwa makamo wake.Guy Scott,mwenye umri wa miaka 70 si mgeni katika siasa za Zambia amechaguliwa kuwa mbunge tangu mwaka 1991 na kuteuliwa kuwa waziri wa kilimo.Amebadilisha uanachama mara kadhaa kabla ya kujiunga na chama cha Sata-Patriotic Front kilichoshinda uchaguzi mwaka 2011.Kwa mujibu wa katiba uchaguzi mkuu unabidi uitishwe katika kipindi cha siku 90,lakini rais wa mpito haruhusiwi kugombea.Ingawa Scott ni mzambia,lakini lakini si kizazi cha tatu -wazee wake wangebidi pia wawe wamezaliwa Zambia ili aweze kugombea.Na mwenyewe anaonyesha kuridhia.Kwa namna hiyo linamaliza kuandika gazeti la Süddeutsche Zeitung,Zambia imeepukana na kishindo kinachoweza kusababishwa na kutawaliwa na rais wa kizungu-hali ambayo ingeweza kuwakumbusha yaliyotokea katika enzi za zamani za ukoloni wa Uingereza.

Sambia Neuer Präsident Guy Scott 6.8.2014
Rais wa mpito wa Zambia Guy ScottPicha: Reuters/Larry Downing

Matumaini yawekewa chanjo dhidi ya Ebola

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu kishindo cha maradhi hatari ya Ebola.Lilikuwa gazeti hilo hilo la kusini mwa Ujerumani Süddeutche Zeitung lililoandika kuhusu maradhi hayo likisema bado hayajadhibtiwa.Hata hivyo linaongeza kusema kiwango cha maambukizi kinaonyesha ni cha chini kuliko ilivyofikiriwa.Matumaini ya raia katika nchi 3 za Afrika Magharibi zinazoathirika zaidi na ugonjwa huo hatari,yaani Liberia,Sierra Leone na Guinea yanawekewa chanjo ambazo mbili zimeshaanza kufanyiwa majaribio.Lakini hata kwengineko barani Afrika watu wanajiwekea matumaini kuona maradhi hayo hatari yanadhibitiwa ili wawekezaji na wataliii wapate kurejea.

Ebola Virus Aufnahme mit Elektronenmikroskop
Virusi vya Ebola vimenaswa na mikroscop ya digital ya elektronikiPicha: Reuters/NIAID

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSE/ALL/PRESSE

Mhariri:Yusuf Saumu