1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi iko tayari kufanya uchaguzi wa bunge

28 Juni 2015

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametaka uchaguzi wa kesho (29.06.2015) ucheleweshwe baada ya upinzani kusema hautashiriki.

https://p.dw.com/p/1Fof5
Burundi Proteste gegen Präsident Nkurunziza
Picha: Reuters/G. Tomasevic

Tume ya uchaguzi ya Burundi imepuuzilia mbali machafuko ambayo yamekuwa yakiendelea kwa wiki kadhaa na kusema iko tayari siku moja kabla uchaguzi muhimu katika taifa hilo la Afrika ya Kati, ambao Umoja wa Mataifa umeonya unapaswa uahirishwe, huku Burundi ikikabiliwa na mzozo mbaya kabisa tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka tisa iliyopita.

"Kila kitu kiko tayari," alisema Pierre-Claver Ndayicariye, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Burundi wakati alipozungumza na waandishi wa habari leo Jumapili. Ndayicariye amesema vifaa vyote vya kupigia kura vimeshapelekwa katika vituo vya kupigia kura, huku kukiwa na vituo zaidi ya 11,000 vya kupigia kura kote nchini.

Upinzani ulisema Ijumaa wiki iliyopita utaususia uchaguzi huo, ukidai haiwezekani kufanya uchaguzi huru, huku watu zaidi ya 127,000 wakiwa wamekimbilia nchi jirani, wakihofia kuzuka kwa machafuko.

Uchaguzi wa bunge na wa serikali za mitaa umepangwa kufanyika siku ya Jumatatu Juni 29 na ule wa rais Julai 15. Wapinzani wanasema nia ya rais Nkurunziza kugombea ni kinyume na katiba na inakiuka mkataba wa amani wa Arusha uliosaidia kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2006 vilivyodumu miaka 13.

Burundi Präsident Pierre Nkurunziza
Rais Pierre NkurunzizaPicha: Getty Images/AFP/F.Guillot

"Vyama vyote vya upinzani vimekubaliana kwa kauli moja kuususia uchaguzi," alisema Charles Nditije, kiongozi wa upinzani mwenye ushawishi mkubwa, katika barua iliyosainiwa na makundi yote ya upinzani ya Burundi iliyoandikwa kwa tume ya uchaguzi.

Lakini Ndayicariye alisema tume haijapokea mawasiliano yoyote rasmi upinzani ukithibitisha kujiondoa katika uchaguzi, ikiwa na maana kwamba uchaguzi ungeendelea bila kucheleweshwa. Kwa hiyo kura watakazopigiwa viongozi wa upinzani zitakuwa halali. "Hili si jambo geni nchini Burundi. Barani Afrika, kususia uchaguzi ni njia nyingine ya kufanya siasa," alisema Ndayicariye. Upinzani uliususia uchaguzi wa mwaka 2010.

Watu watatu wauawa

Watu watatu wameuawa usiku wa kuamkia leo katika mji mkuu Bujumbura, na kuiongoeza idadi ya waliouawa katika wiki kadhaa za machafuko na jaribio la mapinduzi lililosababishwa na azma ya rais Pierre Nkurunziza kugombea awamu ya tatu, kufikia zaidi ya 70.

Kwa mujibu wa Pierre Claver Mbonimpa wa Shirika la kutetea Haki za Binaadamu la APRODH, mtu mmoja aliuwawa katika shambulizi la guruneti na mwingine akapigwa na risasi ya polisi kwanza kabla kushambuliwa na guruneti. Mbonimpa amesema anaamini washambuliaji wanashirikiana na polisi ya Burundi. Mwanajeshi mmoja aliuawa kwa bahati mbaya na mwenzake wakati walipoivamia nyumba moja mjini Bujumbura.

Burundi ilitumbukia katika machafuko mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu wakati rais Nkurunziza alipozindua kampeni yake kuwania awamu ya tatu ya miaka mitano madarakani, hatua iliyozua machafuko yaliyoenea katika sehemu mbalimbali za nchi.

Mwandishi:Josephat Charo/DPA/AFPE

Mhariri:Mohammed Abdulrahman