Ripoti ya HRW yasema wapinzani waandamwa nchini Burundi
18 Mei 2022Shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch limeituhumu Burundi kwamba idara yake ya ujasusi, polisi na wanachama wa tawi la vijana la chama tawala wameshiriki katika matukio ya kuuwa, kuwakamata bila sababu na kuwatesa watu waliodhaniwa kutokea vyama vya upinzani.
Ripoti ya Human Rights Watch kuhusu Burundi imechapishwa leo Jumatano na ina maelezo mengi kuhusiana na matukio mbalimbali yanayoaminika yalifanywa na taasisi za serikali ya Burundi dhidi ya wapinzani wake.
Ripoti hiyo miongoni mwa mengine inataja kwamba mamlaka za nchi hiyo zilijibu mashambulizi dhidi ya raia na mawakala wa serikali yaliyofanywa na makundi ya wenye silaha au watu wanaoshukiwa kuwa waasi, katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa kutumia nguvu kubwa.
Lakini pia inaelezwa mamlaka hazikuonesha kushughulishwa na hatua ya kufanya uchunguzi wa kuaminika, kutafuta ushahidi au kufuata mchakato unaohitajika kuwachukulia hatua wahusika, badala yake katika mikoa ya Cibitoke na Kayanza mwelekeo uliochukuliwa kwa mujibu wa uchunguzi mpya wa Human Rights Watch ni kwamba mamlaka za nchi hiyo ziliwalenga wale wanaokipinga chama tawala CNDD-FDD.
Kufuatia uchunguzi huo Clémentine de Montjoye, mtafiti katika shirika hilo la Human Rights Watch kuhusu Afrika, amesema badala ya serikali ya rais Evariste Ndayishimiye kuwalenga wale wanaoonekana kuwa wapinzani inapaswa kujikita katika kuwafikisha mbele ya sheria waliohusika kwa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu wakiwemo maafisa wa vikosi vya usalama. Amesisitiza kwamba warundi wataacha tu kuishi kwa hofu pale tu wanaoshiriki katika matukio ya kuwahangaisha watakapobebeshwa dhamana.
Shirika la Human Rights Watch liliwahoji watu zaidi ya 30 kati ya Oktoba mwaka 2021 na Aprili mwaka huu, ikiwemo wahanga na mashahidi wa ukiukwaji wa haki za binadamu, watu wa familia za wahanga,pamoja na wawakilishi wa vyama na watetezi wa haki za bindamu nchini Burundi.
Kadhalika shirika hilo lilifanya tathmini na kujiridhisha kwa ushahidi wa kanda ya video iliyowaonesha wanajeshi chungunzima na maafisa wa polisi wakikiri kufanya mauaji. Lakini pia shirika hilo lilifanya tathmini ya ripoti za mashirika ya haki za binadamu ya ndani ya Burundi na ya kimataifa,ripoti za vyombo vya habari sambamba na hotuba zilizotolewa mbele ya hadhara na maafisa wa serikali na taarifa za ujumbe uliochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.
Kutokana na ukubwa wa matukio ya ukikwaji wa haki za binadamu pamoja na kukosekana mashirika ya kutetea haki za binadamu katika eneo hilo, utafiti huu unaweka ukawa umegusia sehemu tu ya ukiukaji unaofanyika katika nchi hiyo.
Vyombo vya habari vya ndani na mashirika ya haki za binadamu ya Burundi pia wamechapishwa matukio ya unyanyasaji katika sehemu mbali mbali za taifa hilo. Kuna simulizi mbalimbali za watu kupotezwa na maafisa wa serikali katika mikoa kadhaa ya nchi hiyo.
Moja ya kisa kilichoelezwa kwa kina ni cha mwanachama mmoja wa chama kikuu cha upinzani Burundi,cha Natonal Congress for Freedom-CNL mwenye umri wa miaka 25 ambaye hajasikika tangu Januari 27 baada ya kupigiwa simu na kwenda kukutana na mwanachama mmoja wa Imbonerankure-ambalo ni tawi la vijana la chama tawala nchini humo katika eneo la Mugina,mkoa wa Citibitoke.
Jamaa zake wanasema wanaume wanne waliokuwa na sare za polisi wakiwa ndani ya gari ambalo linajulikana ni la idara ya taifa ya ujasusi katika mkoa huo waliondoka nae na tangu wakati huo ametafutwa kila pembe hajapatikana ikiwemo polisi.