BVB yaibuka kidedea dhidi ya mahasimu wao wa jadi Schalke
10 Desemba 2018Katika Bundesliga nusu ya pili ya mwaka huu 2018 katika soka la Ujerumani inamilikiwa bila shaka na Borussia Dortmund. Katika mchezo wa 14 kati ya michezo 17 ya duru hii ya kwanza mashati ya BVB yameendelea kubakia safi bila doa.
Imeshinda mara 11 na sare tatu, na bila kushindwa. Washambuliaji wa BVB wameendelea kupata mabao na wana kiwango bora katika ligi hadi sasa , wakipachika wavuni mabao 39, ambapo Paco Alcacer, Marco Reus na wengine wamezisalimia nyavu za timu pinzani bila kusita.
Kocha Lucien Favre ameweza kuunda kikosi imara katika muda wa nusu mwaka , ambacho kinauhakika wa kuwa bingwa wa majira ya mapukutiko na hata kumaliza kipindi hiki ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi.
Borussia Dortmund ilifanikiwa kuangusha Schalke 04 mahasimu wao wa jadi katika mpambano wao siku ya Jumamosi kwa mabao 2-1, ukiwa ni ushindi wao wa kwanza katika muda wa misimu mitano. Borussia Dortmund haijashinda katika mpambano huu wa watani wa jadi dhidi ya Schalke tangu Novemba mwaka 2015 ambapo kutwaa ushindi wa mabao 3-2.
Mara zote Schalke wamekuwa washindi ama timu hizo kutoka sare. Dortmund imeshinda mara 33 hadi sasa kati ya michuano 93 ya Bundesliga dhidi ya Schalke 04 wakati Schalke imeshinda mara 31, na timu hizi mbili zimetoka sare mara 29. Schalke sasa inatofautiana na mahasimu wao hao wa Dortmund kwa pointi 22.
Borussia Moenchengladbach yapanda
Borussia Moenchengladbach imepanda hadi nafasi ya pili katika Bundesliga jana Jumapili baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Stuttgart na katika mchezo wa kwanza Mainz ilitoka sare ya bao 1-1 na Hannover 96. Gladbach imeiondoa Bayern Munich katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi baada ya ushindi huo na kocha wa Gladbach Dieter Hecking aliwaambia waandishi habari za michezo kuwa "tunajiamini tukiwa nyumbani," na kuongeza kwamba "katika kipindi cha pili nilichukua hatua ya kucheza kamari kidogo kwa matumaini ya kuongeza kiwango cha kasi. Nguvu ya kikosi kilichoko katika benchi ni kitu ambacho hatukuwa nacho msimu uliopita."
Ushindi huo wa saba wa Gladbach katika michezo saba ya nyumbani msimu huu umeiweka timu hiyo juu ya bayern na sasa wanaifuta Dortmund nyuma kwa pointi saba.
Timu zinazowania kucheza katika vikombe vya Ulaya , kombe la mabingwa Champions League na Ligi ya Ulaya Europa League ni pamoja na RB Leipzig iliyoko katika nafasi ya 4, ikiwa na pointi 25, licha ya kufungwa mabao 3-0 na Freiburg, wakati Freiburg imejisogeza hadi nafasi ya 12.
Eintracht Frankfurt iko katika nafasi ya 5 ikiwa na pointi 23 licha ya kufungwa bao 1-0 na Hertha Berlin ambayo nayo iko katika nafasi ya 6.
Fortuna Dusseldorf , Hannover 96 na VFB Stuttgart ziko katika nafasi za kushuka daraja, nafasi za 16, 17 na 18.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / dpae / rtre / afpe
Mhariri: Yusuf Saumu