BVB yarejesha mvuto wa Bundesliga
29 Oktoba 2018Sare dhidi ya Hertha Berlin huenda imekuja katika wakati muafaka kwa Borussia Dortmund. Kikosi hicho kimeshindwa mara hii kupachika mabao manne ama zaidi katika mchezo wake pekee katika michezo yake sita iliyopita, mabao 3-0 dhidi ya AS Monaco na iliongoza kwa pointi tatu baada ya kusakata kandanda safi msimu huu.
Ghafla baada ya Bayern Munich kutamalaki katika ligi ya Ujerumani Bundesliga, Dortmund inasaidia kulifanya soka la Ujerumani kuvutia kwa mara nyingine tena.
Kikosi cha kocha Lucien Favre kinafananishwa sasa na kikosi alichounda kocha nyota Juergen Klopp kilichoshinda ligi ya Bundesliga mwaka 2011 na kufuatiwa na ubingwa mwingine mwaka uliofuatia na kushinda kombe la shitikisho DFB Pokal mwaka uliofuatia. Kikosi cha sasa , kama kilivyokuwa cha Klopp , ni cha vijana, kinachofanyakazi kwa nguvu, wachezaji wenye kasi na ufundi, kikijiamini baada ya ushindi wa kupendeza.
Lakini pia kuna ishara za kuimarika baadhi ya timu hali ambayo inaifanya ligi ya Bundesliga kuvutia kwa mara nyingine tena. Werder Bremen ambayo imekuwa ikipata mafanikio katika michezo yake ya hivi karibuni, ilijikuta ikikubali kipigo cha mbwa koko mbele ya Bayer Leverkusen cha mabao 6-2 matokeo ambayo yamewashangaza wapenzi wa kandanda. Werder Bremen ambayo ilikuwa nyumbani ilipata kipigo hicho wakati ilikuwa ikishikilia nafasi ya 2 katika msimamo wa ligi, na sasa imeporomoka hadi nafasi ya 4.
Kohfeldt aelezea kuhusu kipigo
Kocha wa Werder Bremen Florian Kohfeldt ameelezea kipigo hicho kuwa kinatokana na kosa la uchaguzi wa mbinu kuingia katika mchezo huo. Lakini amesema pia kwamba kulikuwa na sababu maalum kuchagua mbinu ya kuwa na walinzi watatu kwa mchezo huo.
Bayern Munich ilipata ushindi wa kibarua dhidi ya Mainz wa mabao 2-1 na kuwa nyuma ya Borussia Dortmund kwa pointi mbili tu ikiwa na pointi 19 ambapo BVB ina pointi 21.
Schalke 04 imesogea hadi nafasi ya 15 baada ya kutoka sare ya bila kufungana na RB Leipzig jana Jumapili na Nuerenberg ilitoshana nguvu na Eintracht Frankfurt kwa kufungana bao 1-1 pia jana Jumapili.
Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 21 ya Ujerumani Horst Hrubesch amelikosoa shirikisho la taifa la kandanda DFB kwa jinsi ya kuwapa mafunzo vijana wenye vipaji, akisema chama hicho kiko nyuma ya mataifa mengine baada ya mafanikio ya hapo awali. "Nimekuwa nikisema kwa miaka mitano kwamba ni lazima tufanye kitu," Hrubesch ameliambia toleo ya Jumatatu la jarida la michezo la Kicker.
"Tuko vizuri hapa DFB lakini tunaweza kufanya vizuri zaidi. Hilo linapaswa kuwa lengo letu , kila mara tuko nyuma hatua moja wakatu tunapaswa kuwa hatua tano mbele. "Chombo cha kutusafirisha tumekikosa lakini tumejibweteka kwa muda mrefu baada ya kizazi cha kila Jerome Boateng, Mats Hummels, Manuel Neuer na Mesut Oezil. Hrubesch mshambuliaji wa zamani wa Hamburg na mshindi wa kombe la mataifa ya Ulaya mwaka 1980 , aliwafunza wachezaji hawa na kupata ubingwa wa vijana chini ya umri wa miaka 21 barani Ulaya mwaka 2009 na kuleta mafanikio makubwa kwa timu ya taifa ya Ujerumani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / dpae / ape / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman