CAF kupata uongozi mpya baada ya FIFA kuingilia kati
8 Machi 2021FIFA imesema makubaliano ya wagombea Augustine Senghor wa Senegal, Jacques Anouma wa Cote d'Ivoire na Ahmed Yahya wa Mauritania kujiondoa kutoka kwenye uchaguzi ujao – na kumuunga mkono Motsepe – yamepatikana baada ya mikutano iliyofanyika Rabat, Morocco wiki iliyopita. Mpango huo ulithibitishwa katika mkutano mwingine wa Jumamosi Mauritania. "Sio siri kuwa CAF imekuwa ikipitia matatizo kadhaa katika nyakati za karibuni. Binafsi nilizungumza na wagombea wote wanne wa urais na marais wengine wengi wa shirikisho. Nnaweza kwa uhakika kuthibitisha kuwa kuna msimamo wa pamoja kati yao, na hicho hatimaye ndio sehemu muhimu ya hilo suala. Kwa hivyo kwa mtazamo wa FIFA tutafanya kazi na CAF kama tulivyokuwa siku za nyuma."
FIFA imesema Motsepe ataongoza CAF kwa kuzingatia na mpango wa pamoja ambao unajumuisha ilani za viongozi hao wote wanne.
Ripoti zinasema Senghor na Yahya watapewa nyadhifa za makamu wa rais na Anouma atakuwa na jukumu la kuwa mshauri wa Motsepe. Motsepe mwenye umri wa miaka 59, ni Tajiri wa uchimbaji madini na mkwe wa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, sasa atachaguliwa kuwa rais wa nane katika historia ya CAF nchini Morocco Ijumaa wiki hii. Itamaanisha atakuwa makamu wa rais wa FIFA. Kizingiti pekee kilichokuwepo kwa Motsepe kimeondolewa baada ya mahakama ya usulishi wa migogoro michezoni CAS kupunguza kutoka miaka mitano hadi miwili adhabu aliyopewa rais wa zamani wa CAF Ahmad Ahmad na kuyamaliza matumaini yake ya kuchaguliwa tena. Ahmad alikutwa na hatia ya kukubali zawadi na mafao mengine pamoja na ubadhirifu wa fedha
AFP, Reuters, DPAE