1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cameron ashinda uchaguzi mkuu wa Uingereza

8 Mei 2015

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, amepata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana nchini Uingereza, baada ya chama chake cha Conservative kujinyakulia viti vingi kwenye uchaguzi huo wa bunge.

https://p.dw.com/p/1FMkm
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron akiwa na mkewe, Samantha
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron akiwa na mkewe, SamanthaPicha: Reuters/P. Noble

Matokeo ya awali yanaonyesha chama cha David Cameron cha Conservative kimepata viti 310 kati ya viti 650 vya bunge la nchi hiyo, huku uchunguzi wa matokeo ya utabiri yakiashiria kuwa chama hicho kitajizolea viti 316.

Chama kikuu cha upinzani cha Labour kimepata viti 217, vikiwa ni viti 25 chini ya idadi iliyokuwa nayo kwenye bunge lililopita, ingawa utabiri unaonyesha kuwa chama hicho kinaweza kujizolea viti 228.

Nacho chama kikuu cha Scotland- Scottish National-SNP, kimefanikiwa kupata viti 58 na hivyo kukosa kiti kimoja tu.

Chama cha Cameron kinatakiwa kupata jumla ya viti 326 ili kuwa na mamlaka kamili ya kuweza kulidhibiti bunge. Shirika la Utangazaji la Uingereza-BBC, linatabiri huenda chama cha Conservative kikapata viti 329. Matokeo yanaonyesha kuwa chama cha Liberal Democrats kimepata viti vinane, baada ya kupoteza viti vyake vingi.

Kura zikiendelea kuhesabiwa
Kura zikiendelea kuhesabiwaPicha: picture-alliance / ZUMA Press

Hata hivyo, kulingana na matokeo hayo, Cameron ana dalili zote za kuendelea kuwa waziri mkuu wa Uingereza kwa miaka mingine mitano. Aidha, Cameron ameibuka mshindi katika jimbo la Oxfordshire. Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Cameron amesema ushindi huo umefanya usiku kuwa mzuri kwa chama chake cha Conservative.

Cameron ataka kuileta pamoja Uingereza

''Zaidi ya yote, nataka kuileta pamoja nchi yetu, Uingereza yetu kwa pamoja, angalau kutekeleza haraka iwezekanavyo masuala ya ugatuzi kama tulivyoahidi na kukubaliana na vyama vingine, kwa Wales na Scotland,'' alisema Cameron.

Cameron amesema anakumbuka mwaka 2010 wakati alipofikia malengo yake ya kukiondoa chama cha Labour na kukirejesha tena madarakani chama chake, kwani ilikuwa ni jambo la kushangaza, lakini kwa ushindi wa leo, huu ni ushindi mzuri kuliko yote. Iwapo utabiri wa matokeo hayo utakuwa sahihi, chama cha Conservative kitakuwa kwenye nafasi ya mbele kuunda serikali ijayo kwa ushirika wa vyama vidogo.

Serikali itakayoongozwa na Conservative, itaendeleza shinikizo lake la kutaka Uingereza kuitisha kura ya maoni ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya ifikapo mwaka 2017. Mchana huu, Cameron anatarajiwa kukutana na Malkia Elizabeth kukubaliana kuhusu mamlaka ya kuunda serikali.

Kiongozi wa Labour, Ed Miliband
Kiongozi wa Labour, Ed MilibandPicha: Getty Images/M. Lewis

Wakati huo huo, kiongozi wa chama cha Labour, Ed Miliband ametangaza nia yake ya kutaka kujiuzulu kukiongoza chama hicho, baada ya kushindwa katika uchaguzi huo. Amesema chama chake kimesikitishwa sana na matokeo hayo. Akizungumza baada ya kushinda katika jimbo la Doncaster, kaskazini mwa Uingereza, Miliband amesema usiku wa kuamkia leo umekuwa mbaya kwa chama cha Labour.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,APE,AFPE,DPAE
Mhariri:Yusuf Saumu