Cameroon na Burundi zatinga fainali za Afcon
24 Machi 2019Nafasi tano zilizobaki zitajazwa leo Jumapili (24.03.2019) ikiwa Afrika kusini ni miongoni mwa mataifa 11 yenye matumaini ya kufuzu kucheza katika fainali zitakazopigwa hapo Juni 21 hadi Julai 19 nchini Misri.
Cameroon ilihitaji sare kutoka katika pambano la kundi B dhidi ya Comoro mjini Yaounde, lakini iliwakandika wakaazi hao kutoka visiwani vya habari ya Hindi kwa mabao 3-0 ambapo nahodha Eric Maxim Choupo-Moting naye alikuwa miongoni mwa wale waliotundika mpira wavuni.
Burundi ni miongoni kwa vikosi vilivyohitaji pointi moja na kufanikiwa kufuzu kwa mara ya kwanza katika fainali hizo za mataifa ya Afrika kwa kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani katika kundi C dhidi ya gabon, ambayo matumaini ya uhai wake yalikuwa ni lazima ishindi mpambano huo.
Namibia ilisherehekea kwa nguvu licha ya kipigo ilichopata katika kundi K cha mabao 4-1 dhidi ya Zambia wakati ikiipiku Msumbiji kutokana na wingi wa magoli na kukata tikiti yake miongoni mwa mataifa 24 yatakayoshiriki katika fainali hizo.
Msumbuji walitarajiwa kufuzu wakati wakiongoza kwa mabao 2-1 dhidi ya Guinea Bissau katika dakika za mwisho lakini hali ilibadilika kutokana na makosa ya walinzi wake ambao waliruhusu timu ya wenyeji kupata sare ya mabao 2-2.
Misri, Algeria, Cote d'Ivoire, Ghana, Guinea, Kenya, Madagascar, Mali, Mauritania, Morocco, Nigeeia, Senegal, Tunisia na Uganda zimekwisha fuzu kabla ya mchezo wa mwisho mwishoni mwa juma hili.
Angola nayo yapita
Angola imejiunga na kundi hilo siku ya Ijumaa wakati walipoishinda Botswana kwa bao 1-0 na kuipiku Burkina Faso iliyojipatia medali ya shaba katika mashindano ya mwaka 2017 na kukamata nafasi ya kwanza katika kundi I.
Baada ya mshambuliaji wa Paris Saint Germain Eric Maxim Choupo-Moting alipowapatia mabingwa mara tano Cameroon uongozi kabla ya mapumziko, Christian Bassong na Clinton Njie walipachika mabao mengine mawili katika kipindi cha pili.
Cameroon ilikuwa taifa lililopangwa kuwa wenyeji hapo kabla mwaka 2019, hali ambayo ingewahakikishia nafasi katika fainali hizo, lakini walishindwa kwenda pamoja na matayarisho ya mashindano hayo na Misri ikachukua nafasi hiyo.
Cedric Amissi aliipa Burundi bao la kuongoza katika dakika ya 75 lakini Omar Ngandu alijifunga mwenyewe muda mfupi baadaye, na kusababisha hali ya wasi wasi kuelekea kumalizika kwa mchezo huo wakati Gabon ilikuwa inasaka goli la pili na kufuzu.
Lakini Pierre-Emerick Aubameyang, nahodha wa wageni hao hakuweza kufungua mlango wa Burundi mjini Bujumbura na kusalim amri miaka miwili baada ya nchi hiyo kuwa wenyeji wa mashindano ya mataifa ya Afrika.
Msumbuji ilikuwa nyuma mjini Bissau na kusawazisha kupitia mchezaji wake Stanley Ratifo na Nelson Divrassone alifikiri bao lake wakati kumebakia dakika moja lingekuwa la ushindi katika mchezo huo.
Lakini mlinzi wa Msumbiji alipiga mpira wa kichwa hovyo kutokana na mkwaju huria wa Guinea-Bissau na mpira huo ukaenda katika nguzo ya goli na Frederic Mendy alichukua hatua haraka na kuutumbukiza wavuni.
Hali hiyo iliiacha Namibia kuwa na furaha kubwa licha ya kufungwa mabao 4-1 katika historia ya soka barani Afrika wakati wakimaliza kwa pointi sawa na Msumbuji, ambao waliwafunga nyumbani na ugenini Oktoba mwaka jana.
Cote d'Ivoire , Mali na Senegal zilishinda michezo yako ambayo haikuwa na uhusiano na kufuzu na Niger ilipigana kutoka nyuma na kutoka sare ya bao 1-1 na mabingwa mara saba wa Afrika Misri.