Cameroon ndio mabingwa wa Afrika
6 Februari 2017Dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika – AFCON mwaka wa 2017 nchini Gabon litakumbukwa kwa kuandikwa hadhiti ya mafanikio yenye kutia moyo wakati Cameroon ilitoka nyuma na kuishinda Misri na hivyo kutwaa taji lake la tano mjini Libreville.
Mashindano mengi tu ya nyuma yalikumbwa na mzigo wa kandanda mbovu, mashabiki wachache wanaofika viwanjani na ukosefu wa uhondo na msisimko uwanjani. Lakini ushujaa wa The Indomitable Lions umehakikisha kuwa dimba la 2017 limekamilika na kuzingatiwa kuwa mojawapo ya mashindano bora zaidi ya karibuni kuwahi kuandaliwa ya kombe la Afrika. Kocha Hugo Broos amekuwa na mahusiano magumu na vyombo vya habari nchini Cameroon tangu alipoteuliwa Februari mwaka jana, na kukosolewa kwa kuwaachanje baadhi ya wachezaji nyota wenye ujuzi na badala yake kuwapa nafasi chipukizi. Huyu hapa Broos "Nnafanya kazi ili kuona matokeo na nna furaha sana kuwa tumeshinda AFCON. Kitu pekee niliwaambia wachezaji na kuwataka wakifanye, kwa sababu tumefanya kazi kubwa katika miezi michache iliyopita, na natumai vyombo vya habari vya Cameroon vilinielewa, ni subira na heshima. Sina tatizo kama mwanahabari atawakosoa wachezaji wangu au chaguo langu, au chochote kile. Lakini unapaswa kubakia na heshima. nadhani sasa wanahabari wa Cameroon wanaelewa hili na sasa uhusiano baina yetu tayari umeimarika kuliko ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita".
Na mara hii Simba wa Nyika waliweza kuwakwaruza mapharao. Kocha wa Misri Hector Cuper alisema inauma sana kuwa walipoteza fainali hiyo. "Kwanza kabisa, naipongeza Cameroon kwa kushinda kombe hilo. Wameonyesha mchezo mzuri na walistahili kushinda. Bila shaka nimekasikitishwa na kichapo, lakini nawahurumia sana watu wa MISRI. Nilitaka sana wafurahie leo na kushinda kombe hili kwa ajili yao kwa sabbau nafahamu walilihitaji sana. Na pia kwa wachezaji kwa sababu wamepambanana sana hadi mwisho. Lakini walishindwa kucheza kwa kiwango cha juu kwa dakika 90".
Na sasa kwa mengi zaidi kuhusu namna fainali ilivyokuwa pamoja na dimba lenyewe kwa jumla, naungana kwa njia ya simu na mwanaspoti David Kwalimwa ambaye amelifuatilia dimba hilo tangu lilipoanza mjini Libreville,
Cameroon ambayo sasa ina mwonekano mpya imeubeba maramoja wa matarajio maana wao ndio mabingwa wa Afrika. Wataandaa dimba lijalo mwaka wa 2019 ambapo mashabiki wa nyumbani watataka kuona marudio ya mafanikio waliyopata GABON.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP
Mhariri: Gakuba Daniel