Cape Verde yatinga robo fainali
28 Januari 2013Leo(28.01.2013) ni zamu ya jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, mabingwa wa zamani Ghana , Niger, na Mali kuwania nafasi mbili za robo fainali.
Filamu za Disney ni maarufu kutokana na kuwafanya viumbe dhaifu kuwa na nguvu na kupata ushindi kwa hali ambayo huwezi kuamini, lakini hata watayarishaji wa filamu hizo hawangeweza kufikiria jinsi Cape Verde walivyoweza kupata mafanikio kila mara katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika.
Kwanza walipata tikiti ya kuingia katika fainali hizi huko Afrika kusini baada ya kuuangusha mbuyu , mabingwa mara nne wa kombe la mataifa ya Afrika Cameroon mwaka jana , katika ushindi uliowashangaza wengi katika bara hilo.
Taifa hilo dogo kabisa kuweza kufanikiwa kuwakilishwa katika fainali hizi za kombe la mataifa ya Afrika , likiwa na wakaazi nusu milioni, Cape Verde lilionyesha katika mchezo wa ufunguzi kuwa matokeo yake dhidi ya Cameroon hayakuwa ya kubahatisha. Kikosi hicho kinachopatiwa mafunzo na kocha Lucio Antunes kilitoka sare ya bila kufungana na wenyeji wa mashindano hayo Afrika kusini mwanzoni mwa mashindano haya mjini Johannesburg.
Walihamia baadaye mjini Durban ambako walitiana kifuani na Morocco na kutoka sare ya bao 1-1, ambapo goli la kusawazisha la Simba hao wa milima ya Atlas lilikuja katika dakika ya 78.
Mchezo huo ulimalizika kwa sare , na kuwaacha Papa hao wa Bluu , wakihitaji kushinda dhidi ya Angola iwapo watahitaji kuingia katika robo fainali.
Ghana yachungulia robo fainali
Ghana ina nafasi kubwa ya kuingia katika duru ya robo fainali katika kundi B, ikiwa na points 4 ambapo pia zimo timu za Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo , Niger na Mali. Mali ina points 3 na DRCongo ina points 2 wakati Niger ina point moja. Iwapo Niger itaifunga Ghana leo jioni , itakuwa na points sawa na Ghana na Mali itakuwa katika nafasi nzuri iwapo itaishinda DRCongo.
Bayern yapeta
Na katika ligi za hapa barani Ulaya, Bayern Munich ilifanikiwa kuwaweka mbali wapinzani wake pale ilipoweza kuipa kipigo VFB Stuttgart kwa kuichapa mabao 2-0 jana Jumapili ikiweka mwanya wa points 11 baina yake na timu inayofuatia ya Bayer Leverkusen ambayo nayo ilitoka sare ya bila kungana na FC Freiburg siku ya Jumamosi ikiendelea kushika nafasi ya pili kwa kuwa na points 37. Mabingwa watetezi Borussia Dortmund inashikilia bado nafasi ya tatu ikiwa na points 36.
Wakati huo huo mkurugenzi wa sporti katika Bayern Munich Matthias Sammer ameitaka timu yake kupandisha kiwango chake. Baada ya kipindi cha kwanza ambacho hakikuwa na mvuto , Bayern ilikuja juu na mshambuliaji kutoka Croatia Mario Mandzukic kupachika bao kabla ya kummegea pasi Thomas Muller na kuandika bao la pili.
Lakini baada ya kuiona timu yake ikisumbuka kupata ushindi wa mabao 2-0 mjini Munich dhidi ya klabu iliyomkiani mwa ligi Greuther Feurth, Sammer alisema lazima Bayern ipandishe kiwango chake. Tulicheza vizuri lakini kuwa wazuri tu hakutoshi kwa ajili ya msimu mzima.
Messi anatisha
Lionel Messi alipachika mabao 4 na Cristiano Ronaldo alipata mabao matatu wakati vigogo hao wa soka la Uhispania , Barcelona na Real Madrid wakijipasha moto misuli kwa ajili ya pambano lao la el clasico katika nusu fainali ya kombe la chama cha soka cha Hispania siku ya jumatano. Barcelona ilishinda Osasuna kwa mabo 5-1, wakati Real ilipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Getafe.
Wakati huo huo Atletico Madrid ambayo inashikilia nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ya Hispania iliteleza jana na kupata kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Athletic Bilbao. Kutokana na kipigo hicho Barcelona sasa imepanua mwanya na sasa inaongoza kwa points 11 kutoka timu hiyo iliyoko nafasi ya pili. Madrid iko nafasi ya tatu.
Huko Ufaransa Paris Saint Germain imerejea kileleni katika ligi ya daraja la kwanza nchini humo jana Jumapili, kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Lille, katika uwanja wa Parc des Princes.
Goli alilojifunga mwenyewe mlinzi kutoka Cameroon Aurelien Chedjou lilitosha kuipa ushindi PSG.
Nchini Italia, Napoli imejisogeza masafa ya points tatu karibu na viongozi wa ligi ya Italia, Serie A wakati Parma iliposhindwa kuendeleza ubabe wao nyumbani jana Jumapili. Juventus ilitaraji kupanua mwanya wa points , lakini ilikataliwa na Sampdoria Genoa na kutoka sare ya bao 1-1 siku ya Jumamosi. Napoli ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Parma ambayo ilikuwa haijashindwa nyumbani msimu huu hadi jana.
Premier league kesho
Katika Premier league nchini Uingereza Manchester City ambayo ilikuwa nyuma ya mahasimu wao Manchester United kwa points saba kuanzia Januari 18 , inaweza kupunguza mwanya huo hadi points mbili iwapo itapata ushindi dhidi ya Queens Park Rangers kesho Jumanne. Hata hivyo United inaweza kurejea katika nafasi yake hiyo kwa ushindi dhidi ya Southampton siku ya Jumatano, lakini safari ya City katika timu hiyo ambayo iko mkiani mwa ligi ya Uingereza inatoa nafasi kuweza kuleta msisimko katika mbio za ubingwa katika Premier League.
Wakati huo huo Klabu ya Galatasaray ya Uturuki imefikia makubaliano na mshambuliaji wa Cote D'Ivoire Didier Drogba ya mkataba wa miezi 18. Drogba aliondoka Chelsea baada ya kuisaidia timu hiyo kunyakua taji la Champions League mwaka jana na kujiunga na klabu ya China ya Shnghai Shenhua.
Tennis:
Novak Djokovic amekuwa tena bingwa wa mashindano ya Australia open baada ya kumshinda Andy Murray kwa seti 3-1 kwa 6-7 , 7-6, 6-3, na 6-2. Djokovic ameweka rekodi sasa ya ushindi mara tatu katika Australian open.
Na katika ngumi:
Bingwa wa mkanda wa baraza la ngumi duniani na chama cha mchezo wa ngumi duniani Danny Garcia katika uzito wa junior ameahirisha pambano lake lililopangwa kufanyika Februari 9 dhidi ya Zab Judah na sasa litafanyika hapo Aprili 27. Garcia alilazimika kusogeza mbele pambano hilo kutokana na kuumia mbavu wakati wa mazowezi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /dpae
Mhariri: Mohammed Khelef